Takriban watu 34 wamepoteza maisha baada ya Kimbunga Chido kupiga nchini Msumbiji tangu siku ya Jumapili, Shirika la Umoja wa Mataifa la misaada ya kibinadamu OCHA lilisema Jumanne, likinukuu takwimu za Shirika la Maafa la nchi hiyo ya Kusini mwa Afrika.
"Hadi kufikia tarehe 17 Disemba 2024, jumla ya watu 174,158 walikadiriwa kuathiriwa na kimbunga, na watu 34 walipoteza maisha na wengine 319 kujeruhiwa," imesema OCHA katika taarifa yake.
Athari ya Kimbunga Chido Mayotte
Kisiwa kidogo cha Ufaransa cha Mayotte kilikumbana na dhoruba hiyo, huku maelfu wakiaminika kupoteza maisha kabla ya kuhamia Msumbiji kwenye pwani ya mashariki ya kusini mwa Afrika.
Mamlaka mjini Mayotte wana changamoto ya upungufu wa lishe na kuenea kwa magonjwa katika eneo la ng'ambo la Ufaransa baada ya kimbunga kikali cha Chido kupiga mwishoni mwa juma lililopita.
"Mpaka sasa maelfu wanakadiriwa kupoteza maisha katika mji wa Mayotte, baada ya kimbunga Chido," wanasema maafisa wa Ufaransa.
Dhoruba hiyo imeharibu sehemu kubwa za visiwa karibu na Afrika mashariki, eneo ambalo liko chini ya uongozi wa Ufaransa, kabla ya kukumba maeneo mengine ya Afrika.
Maeneo mengi ya Mayotte bado hayawezi kufikiwa na baadhi ya waathirika waliozikwa kabla ya takwimu kuthibitishwa inaweza kuchukua siku kadhaa kudhihirisha kiwango kamili cha uharibifu huo.
Kufikia sasa, vifo 22 na zaidi ya majeruhi 1,400 vimethibitishwa.
"Kipaumbele leo ni maji na chakula," alisema Ambdilwahedou Soumaila, Meya wa mji mkuu Mamoudzou na kuongeza, "Kuna watu wamefariki kwa bahati mbaya ambapo miili inaanza kuoza ambayo inaweza kuleta tatizo la kiafya."