Shirikisho la Soka Barani Afrika (CAF) limemsimamisha kazi Adel Amrouche, kocha wa timu ya taifa ya Tanzania kwa mechi nane, kufuatia kauli yake dhidi ya timu ya taifa ya Morocco.
Wakati huo huo, Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limemuweka kando kocha huyo raia wa Algeria, na nafasi yake ikichukuliwa na wazawa, Hemed Morocco na Juma Mgunda.
Amrouche, ambaye anaiongoza ‘Taifa Stars’ kwenye michuano ya AFCON inayoendelea huko Ivory Coast, aliibua sintofahamu baada ya kudai kuwa timu ya Morocco na Shirikisho lao la Soka (RMFF), yanapewa upendeleo maalumu kwenye michuano mbalimbali barani Afrika.
Katika kuondoa utata kwenye kauli yake ya awali, akizungumza muda mchache kabla ya Tanzania kuminyana na Morocco, Amrouche alikimwagia sifa kikosi cha ‘Simba wa Atlas, akikielezea kuwa ni mojawapo ya timu bora zaidi duniani.
Hata hivyo, Morocco ikaibuka mshindi kwa kuicharaza Tanzania mabao matatu bila katika mchezo wa ufunguzi wa kundi F uliofanyika katika uwanja wa Laurent Pokou, mjini San-Pedro.