Maoni chanya yametawala ufunguzi wa AFCON 2023, huku Rais wa CAF Patrice Motsepe akiita ''tamasha linalounganisha Afrika nzima.''
Kwa upande wake Yemi Alade mwanamuziki maarufu kutoka Nigeria, ambaye pia ameshiriki kwenye wimbo huo amelielezea tukio hilo kama 'ndoto iliyotimia.'
“Toka 2016, nilitamani kujiona nikitumbuiza kwenye matukio makubwa yanahusu soka, nikizungukwa na mamia ya wachezaji na mashabiki wengine.
“Na leo, miaka saba baadaye natumbuiza kwenye jukwaa la AFCON, hakika ni heshima sana kwangu kwani ndoto yangu imetimia. Na huu ni mwanzo tu," alijinasibu msanii huyo kwenye ukurasa wake wa X.
Waandaaji wa michuano hiyo mikubwa wamefanikiwa kuleta burudani mujarab ikiwa ni sehemu ya kufurahia asili ya Afrika na soka maridhawa.
Hata maandalizi kuelekea tamasha la ufunguzi wa michuano hiyo, yalipata idadi kubwa ya wafuatiliaji kwenye mitandao ya kijamii, huku Mohamed Ramadan msanii kutoka Misri, akiweka wazi kuwa akaunti yake ya You Tube ilivuka watazamaji bilioni 500.
Msanii huyo pia alishiriki kwenye wimbo huo, 'Akwaba', akiwa na Yemi Alade.
"Akwaba", ikimaanisha karibu kwa lugha ya Baoulé, ndio wimbo rasmi wa michuano hii, ukiwa umetungwa na kikundi cha Magic System kutoka Ivory Coast na kuzalishwa na mshindi wa tuzo za Grammy na Mwanamuziki kutoka Congo, Danny Synthe.
‘’Africa iko tayari,’’ aliandika Ramadan kwenye ukurasa wake wa Facebook, huku akiwashukuru mashabiki kwa uchangamfu waliouonyesha wakati wa ufunguzi wa AFCON 2023.
Hadi sasa, wimbo wa Akwaba umejikusanyia watazamaji zaidi ya milioni tano kwenye ukurasa wa You Tube.
Kwa mujibu wa Universal Music Africa(UMA), kampuni ya kuzalisha muziki barani Afrika, bado zipo nyingi zenye maudhui ya AFCON ambazo hazijawekwa hadharani.
‘’Ili kuongeza nakshi kwenye michuano hii, tumeleta pamoja wasanii 15 wenye vipaji, na wengine saba ambao wamebobea katika kutengeneza mirindimo, itakayowapa burudani stahiki Waafrika wote,’’ iliandika UMA kwenye ukurasa wake wa Instagram.
Mwezi uliopita, idadi ya nyimbo zenye kuzungumzia AFCON 2023 ziliwekwa kwenye mitandao kadhaa.
Walioshirikishwa kwenye nyimbo hizo ni kama vile Serge Beynaud, Kerozen na Josey.