Kocha huyo raia wa Algeria, amekimwagia sifa kikosi cha timu ya taifa ya Morocco, kitakachokutana na 'Taifa Stars', kwenye ufunguzi wa michezo ya kundi F, utakaochezwa kwenye uwanja wa Laurent Pokou, mjini San-Pedro, nchini Ivory Coast.
“Timu ya Morocco inajieleza yenyewe … ni mojawapo ya timu bora zaidi duniani,” alisema Adel Amrouche, akilisifia benchi la Morocco.
Mwalimu huyo ambaye kikosi chake kinashiriki kwa mara ya tatu katika mashindano ya AFCON, alihusisha mafanikio na kiwango cha kimataifa cha timu ya taifa ya Morocco na historia ya nchi hiyo, na sio 'bahati', kama alivyodai mwanzoni.
Kocha Amrouche aliibua sintofahamu kufuatia kauli yake ya awali, alipodai kuwa Shirikisho la Soka la Morocco (FRMF) lilikuwa na 'mkono wa ushawishi' kwenye uendeshaji wa mpira wa miguu barani Afrika.
Hata hivyo, kocha wa Morocco Walid Regragui aliyatupilia mbali madai hayo, akisisitiza kuwa akili yake yote iko kwenye mchezo huo.
Wakati huohuo, kocha Amrouche amejinasibu kuwa kikosi cha Taifa Stars kipo tayari kwa mchezo huo na kwamba wanategemea kupata matokeo mazuri baada ya mtanange huo.
Kwa mujibu wa mkufunzi huyo, wachezaji wake wamedhamiria kuweka historia kwenye michuano ya mwaka huu, kwa kucheza vizuri mechi zao zote kwenye kundi F.
"Utakuwa mchezo mgumu kwetu na tuko hapa kushindana hasa ukizingatia tunakutana na mpinzani mgumu," alisisitiza.
Timu hizo zilikutana kwa mara ya mwisho Novemba, 2022 katika mchezo wa kufuzu Kombe la Dunia 2026, kundi E, uliofanyika Uwanja wa Benjamin Mkapa Jijini Dar es Salaam, Tanzania ambapo Morocco waliibuka washindi kwa mabao mawili kwa bila.