Timu ya Taifa ya mpira wa miguu ya Tanzania (Taifa Stars) imepanga kupiga kambi nchini Misri kujiandaa na michuano ya fainali za Afcon zinazoanza mapema Januari mwaka 2024 huko Ivory Coast.
Kambi hiyo itaanza Disemba 30 mwaka 2023, siku tatu baada ya mechi maalumu ya kuzindua Uwanja wa Amaani Stadium utakaozikutanisha timu za Tanzania Bara Kilimanjaro Boys na Zanzibar, Zanzibar Heroes siku ya Jumatano tarehe 27 Disemba.
Kambi hiyo itakayochukua takriban wiki 2 nchini Misri inategemea kumpa nafasi kocha mkuu wa kikosi hicho cha taifa Adel Amrouche, kuwanoa wachezaji wake na kuwaweka tayari kwa mashindano makubwa zaidi ya soka barani Afrika.
Taifa Stars imepangwa kundi F ikiwa pamoja na Morocco, DRC na Zambia.
Mechi yao ya ufunguzi katika michuano hiyo mikubwa barani kwa timu za taifa watacheza dhidi ya Morocco, Januari 17 katika dimba la San-Pedro Stadium.
Kocha mkuu wa Taifa Stars Amrouche, tayari ametangaza majina ya wachezaji 53 kama ni kikosi cha awali kabla ya uchaguzi makini wa wachezaji atakaowatumia kwenye kinyang’anyiro hicho.
Jumla ya wachezaji 24 wanaocheza soka nje ya nchi katika vilabu mbali mbali wameitwa kwenye kikosi hicho cha taifa.
Orodha hiyo ya wachezaji imetawaliwa na wachezaji wa Yanga SC, huku Simba SC na Azam FC zikitoa wachezaji 4 tu kila timu.