Wizara ya afya nchini Kenya imeagiza baraza la madaktari na wahudumu wa afya (KMPDC) kutekeleza kufungwa mara moja kwa kliniki za urembo ambazo hazijasajiliwa na zinazofanya kazi kinyume cha sheria.
Wizara ya afya imesema jumla ya kliniki 26 za urembo zilifanyiwa tathmini, 20 zilionekana kukidhi viwango vya uendeshaji lakini vituo vitatu vilituma maombi ya kusajiliwa na vilikuwa vinasubiri kuidhinishwa huku vingine vitatu vikifanya kazi kinyume cha sheria bila kusajiliwa.
" Kliniki zote zote zilizo na utaratibu duni wa kuzuia na kudhibiti maambukizi lazima zifuate utaratibu unaopendekezwa ndani ya siku 30," wizara imesema katika taarifa.
Wizara imeagiza kuwa vituo visivyo na utaratibu wa matibabu ya dharura lazima vianzishe na kuandaa huduma za dharura ndani ya siku 60.
Uchunguzi wa wizara katika vituo vya urembo 102 ulionesha kuwa saba vilikuwa vinatoa huduma kama ya kuchora nyusi na kutumia sindano kwa watu bila utaratibu unaotakiwa.
Wizara ya afya imeagiza kuwa vituo vya urembo ambavyo havijazingatia taratibu za uendeshaji lazima vifanye hivyo ndani ya siku 60 ili kuhakikisha mazingira salama ya kuhudumia watu.
Spaa zote za urembo na matibabu haziruhusiwi kutoa au kutangaza utaratibu wa kimatibabu ambao unahusu uchomaji sindano au upasuaji wa aina yoyote, kwa kukata au kutoboa ngozi au kwa kuingiza vifaa ndani ya mwili.