Serikali ya Kenya, mara kadhaa, imelinusuru shirika la ndege la taifa la Kenya Airways. / Picha: Reuters

Shirika la ndege la Kenya Airways lililokumbwa na matatizo lilisema Jumanne kuwa lilikuwa limeandikisha faida ya uendeshaji mwaka wa 2023, ikiwa ni ya kwanza katika kipindi cha miaka saba.

Kiasi cha shilingi bilioni 10.5 za Kenya (kama dola milioni 80) kwa mwaka uliomalizika Desemba 31 inawakilisha mabadiliko makali kutoka kwa hasara ya uendeshaji ya shilingi bilioni 5.6 mwaka wa 2022, huku mwenyekiti Michael Joseph akiisifu kama "hatua muhimu."

Shirika hilo la ndege, ambalo mwanahisa wake mkubwa ni serikali ya Kenya, pia lilisema katika taarifa kwamba hasara yake baada ya ushuru imepungua hadi karibu shilingi bilioni 23 kutoka zaidi ya shilingi bilioni 38 mwaka uliopita.

Jumla ya mapato kwa mwaka yalipanda kwa 53% hadi shilingi bilioni 178, ambayo shirika hilo lilihusisha zaidi na ukuaji wa 35% wa idadi ya abiria hadi milioni 5.04, kulingana na taarifa yake ya matokeo iliyokaguliwa.

Mlima wa deni

Shirika la ndege la Kenya Airways limekuwa likifanya kazi chini ya mlima wa madeni na hasara kwa miaka mingi licha ya misaada mingi ya serikali, na kama sekta ya usafiri wa anga kwa ujumla iliathiriwa sana na janga la COVID-19.

"Takwimu hizi zinaangazia utendaji wa ajabu wa shirika la ndege kwa mwaka mzima na kutoa dalili za kutia moyo za kuendelea kuimarika katika sekta ya usafiri wa anga," Joseph alisema katika taarifa.

"Pia zinathibitisha uwezekano wa uendeshaji wa biashara ya ndege na kuonyesha kwamba juhudi zinazoendelea za usimamizi kurejesha faida zinaleta matokeo chanya."

Mkurugenzi Mtendaji Mkuu Allan Kilavuka alisema lengo la kampuni kwa muda mfupi lilikuwa kukamilisha "mpango wa urekebishaji mtaji ambao malengo yake makuu ni kupunguza wigo wa kifedha wa kampuni na kuongeza ukwasi."

Safari kwa maeneo 45 duniani

Serikali inamiliki asilimia 48.9 ya hisa za Kenya Airways, huku Air France-KLM ikiwa na asilimia 7.8%.

Shirika hilo la ndege lilianzishwa mwaka 1977 kufuatia kufariki kwa shirika la ndege la East African Airways na sasa linasafiri kwa safari 45 duniani kote, 37 kati yao zikiwa barani Afrika.

TRT Afrika