Rais William Ruto anataka kufanyike mkutano wa dharura wa viongozi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, EAC, kujadili hali ya usalama katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC.
Kenya ni Mwenyekiti wa EAC wa mwaka huu.
" Baada ya kushauriana na wakuu wa nchi wanachama wa EAC, tutaitisha mkutano wa haraka wa viongozi, ndani ya muda wa saa 48 zijazo ili kutafuta suluhu ya mzozo huu ," Rais William Ruto alisema katika taarifa.
Mashambulizi mapya ya kundi lenye silaha la M23 Mashariki mwa DRC yamezua hofu huku maelfu wakilazimika kuhama makazi yao.
"Ghasia zinazoendelea Kivu ya Kaskazini zinatishia kuiingiza Mashariki mwa DRC katika janga kubwa zaidi. Idadi ya watu waliokimbia makazi yao imeongezeka hadi kufikia 400,000 mwaka huu pekee," Rose Tchwenko, Mkurugenzi wa Shirika la misaada la Mercy Cops nchini DRC amesema.
"Goma ni zaidi ya mji mkuu wa kikanda--ndio mhimili wa shughuli za misaadai kote Mashariki mwa DRC, na ukubwa wa mgogoro huu mpya unatishia kulemea uwezo wake. Baada ya miaka mingi ya kubeba mzigo mkubwa wa migogoro isiyokoma, Goma sasa inakaribia kushindwa kuhimili tena," Tchwenko ameongezea.
Umoja wa mataifa ulifanya mkutano wa dharura 26 Januari 2024 kujadili tishio la kundi la M23 nchini DRC.
Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ametoa wito kwa majeshi ya Rwanda kuondoka ndani ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na kusitisha msaada kwa wapiganaji wa M23 wanaoelekea kwenye mji muhimu wa Goma Mashariki mwa nchi hiyo.
Guterres "ameendelea kulaani vikali uvamizi unaoendelea wa kundi la M23 wakielekea Goma huko Kivu ya Kaskazini kwa msaada wa vikosi vya Rwanda," msemaji wake Stephane Dujarric alisema katika taarifa Jumapili.
Lakini Rwanda imekanusha madai hayo ambayo yanaunngwa mkono na DRC pia.