Na
Abdulwasiu Hassan
Hili hapa ni swali la haraka: Kuna uhusiano gani kati ya nguo za Nigeria na taifa hilo la Afrika Magharibi kuibuka kama timu ya soka yenye nguvu?
Mashabiki wa mchezo huo wakiwa na jicho la kina wanaweza kukumbuka kwamba mfungaji bora wa wakati wote wa Super Eagles, marehemu Rashidi Yekini, alianza uchezaji wake katika klabu ya United Nigeria Textiles Ltd (UNTL) FC katika jiji la kaskazini la Kaduna mnamo 1982.
Hiki ndicho kipindi ambacho makampuni mengi ya kibinafsi yalifadhili vilabu vya soka vya humu nchini, hivyo kuchangia ukuaji wa mchezo huo katika nchi ambayo siku zote ilikuwa na hazina kubwa ya vipaji lakini kulikuwa na raslimali chache za kukuza vipaji hivyo.
Jambo la kushangaza ni kwamba, kuzorota kwa sekta ya nguo iliyowahi kustawi nchini Nigeria kuliambatana na Super Eagles kupanda katika mashindano ya kimataifa, ikiwa ni pamoja na kushinda Kombe la Mataifa ya Afrika mwaka wa 1994 na medali ya dhahabu ya Olimpiki mwaka wa 1996.
Katika muongo huo huo, kampuni za nguo nchini zilikabiliwa na hatari kubwa, na hatimiye kufilisika moja baada ya nyingine.
Utafiti unaonyesha kuwa kati ya mwaka 1994 na 2005, takriban asilimia 64 ya makampuni ya nguo yaliyosajiliwa nchini Nigeria yalifilisika, na hivyo kushusha idadi hiyo chini kutoka 125 hadi 45 katika kipindi cha miaka kumi na moja tu.
Kufikia 2022, kulikuwa na chini ya kampuni 20 za nguo zilizokuwa zikifanya kazi. Mnamo 1985, kulikuwa na kampuni kama hizo 175 zenye faida kubwa zilizoajiri maelfu ya wafanyikazi.
"Kwa kuzingatia ajira, idadi ya ajira zilizoundwa na sekta hiyo ilipungua kutoka 137,000 mwaka 1996 hadi 24,000 mwaka 2008. Kufikia 2022, kulikuwa na ajira chini ya 20,000 katika sekta hiyo," anasema Folorunsho Daniyan, rais wa Chama cha Watengenezaji Nguo cha Nigeria. (NTMA).
Sababu za kufilisika
Hamma Kwajaffa, mkurugenzi mkuu wa NTMA, anafuatilia kuporomoka kwa sekta ya nguo ya Nigeria hadi kuanguka kwa naira katika miaka ya 1980. Watengenezaji wa nguo waliokuwa na mikopo ya nje ya kulipa walibeba mzigo mkubwa.
"Ulipaji wa mikopo ulizidi kuwa tatizo kutokana na marekebisho ya viwango vya ubadilishaji wa fedha za kigeni," anaiambia TRT Afrika.
"Kutoka dola moja ya Marekani ilipokuwa Naira 3 dola ya, kiwango cha ubadilishaji kilipanda hadi Naira 30 ilipofika1985. Hali ya maisha yakawa magumu".
Tatizo la fedha lilichangiwa na wazalishaji wa ndani kushindwa kushindana na vitambaa vya bei nafuu vilivyotengenezwa nje ya nchi ambavyo vilianza kuingia nchini.
"Uchumi huria, wa soko huria ulisababisha bidhaa za duni kuingizwa nchini na hata bidhaa za magendo za bei nafuu hadi Nigeria, kwa bei ya chini sana kushinda bei ya gharama ya bidhaa za nguo za ndani. Hiki kilikuwa kichochezi cha kushuka taratibu ambako kulisababisha kuporomoka kwa jumla kwa biashara hio," anasema Kwajaffa.
Lakini Abubakar Musa Bunza, mhadhiri katika idara ya polima na uhandisi wa nguo katika Chuo Kikuu cha Ahmadu Bello huko Zaria, anaona tatizo hilo kwa mtazamo mpana.
Anahusisha kuporomoka kwa sekta hiyo na mambo kama vile ukosefu wa umeme endelevu na wa bei nafuu, rushwa, na migogoro kati ya vyama vya wafanyakazi na waajiri.
Bunza anaamini kuwa tasnia ya ndani pia iliteseka kwa kukosa malighafi bora, kukosekana kwa wakala rasmi wa kufuatilia sekta hiyo, na madai ya serikali zilizofuata kutoweza kutatua matatizo haya.
Mipango ya kufufua iliyofeli
Sekta hii imekuwa ikianguka kwa muda mrefu licha ya uingiliaji wa mara kwa mara wa serikali.
Katika miaka ya hivi karibuni, serikali ya Rais wa zamani Goodluck Jonathan ilitoa mikopo ya jumla ya bilioni N60 kwa ajili ya kufufua sekta ya nguo. Utawala wa zamani wa Muhammadu Buhari, pia, uliunda hazina ya bilioni N294, lakini haikuleta tofauti hata kidogo.
Makamu wa Rais Kashim Shettima alisema hivi karibuni kwamba utawala wa sasa wa Bola Ahmed Tinubu unashirikiana na Kamati ya Kimataifa ya Ushauri wa Pamba (ICAC) kufufua sekta hiyo na kuunda nafasi za kazi milioni 1.4 kila mwaka.
"Utawala wa Tinubu utafanya juhudi za kuhakikisha nchi inatumia fursa katika thamani ya pamba, ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kwamba Nigeria inarejesha uanachama wake wa ICC," alisema.
Wakati Shettima hakuingia kwa undani kuhusu chanzo cha fedha za mpango huu wa ufufuaji, waziri wa biashara na uwekezaji Doris Uzoka-Anite alisema Nigeria imepata uwekezaji wa dola bilioni 3.5 kwa sekta hiyo.
Wito wa kutumia mbinu mpya
Sio kila mtu anavutiwa na matamshi ya serikali ya shirikisho, kutokana na historia ya mipango kama hiyo.
"Mpaka suluhu la matatizo lisipopatikana, uingiliaji kati wowote unaweza kushindwa," Bunza anaiambia TRT Afrika.
"Suluhu zinazohitajika ni pamoja na umeme wa bei nafuu na endelevu, sera ya usawa ya kuagiza-usafirishaji bidhaa ambayo itapendelea watengenezaji wetu wa nguo, na wasomi wanaoshirikisha kwa utafiti." Mhadhiri wa chuo kikuu pia anapendekeza kuundwa kwa baraza la utafiti wa nguo.
Mkurugenzi mkuu wa NTMA Kwajaffa anaamini kuwa Nigeria inahitaji kuchukua mfano kutoka kwa mataifa mengine yanayoibukia ambayo viwanda vyake vya nguo vinafanya kazi.
Athari ya sarafu iliyopunguzwa thamani
Tangu kuanguka kwa naira ya Nigeria mwaka 2023, sarafu hiyo imepoteza zaidi ya nusu ya thamani yake -kutoka N700 kuwa sawa na dola moja hadi kufikia N1,600 kwa dola moja .
"Kama tutashusha thamani ya naira, tutakuwa taifa la watumiaji. Itatufanya tusiwe na ushindani, na hatutaweza kuuza nje," Kwajaffa anaiambia TRT Afrika.
Bunza anaonyesha kuwa kushuka kwa thamani ya sarafu kunaathiri vibaya uagizaji wa malighafi na vifaa.
Hajia Aisha Mohammed, ambaye ana duka mjini Abuja, anasema mahitaji ya nguo yamepungua kwa sababu ya bei ya juu ya vitambaa kutoka nje ya nchi.
Vitambaa vilivyokuwa vya bei nafuu, sasa ni ''ghali," anaiambia TRT Afrika.
Baadhi ya wachambuzi wanaona kuwa tasnia ya nguo ya ndani inahitaji kubadilisha mbinu, kutafuta soko la vitambaa nje ya Afrika, na kuondoka Nigeria.