Na Mamadou Thiam
Ndoto kubwa ya kuwa na kesho iliyo bora zaidi inasukuma maelfu ya vijana wa Kiafrika kujaribu janga la uhamiaji haramu.
Modou Thiaw anajua gharama mtu anayotakiwa kulipa hata ikibidi kuhatarisha maisha yake kutafuta kile ambacho ni kwa kawaidi ni vigumu kupatikana, baada ya kujaribu mara mbili bila mafanikio ya kuvuka bahari kutafuta maisha bora ambayo kimsingi hakuwa na uhakika angeyapata.
Akiwa amekamatwa nchini Algeria baada ya kupita Mauritania, mzaliwa huyu wa Touba Toul katika eneo la Thiès alipitia hatari nyingi katika jangwa la Niger kabla ya kurejeshwa nchini Senegal.
Akiwa na umri wa miaka 40, sasa anajaribu sio tu kujenga upya maisha yake bali pia amekuwa sauti ya wahamiaji waliorudishwa makwao, akiuambia ulimwengu juu ya mapambano ya maelfu ya vijana wa Senegal yanayoendeshwa na msukumo wa kukaidi bahari na mawimbi yake hatari.
"Kufanikiwa kusaidia familia zetu au kuungana katika umauti na wale ambao wametangulia mbele ya haki!" hii ilikuwa kauli mbiu ya Modou alipofanya uamuzi wa kuondoka Senegal na kuelekea Ulaya. Hio ilikua mwaka 2008.
Baada ya kukaa gerezani kwa muda mfupi - alikamatwa wakati wa zoezi la mamlaka dhidi ya wachuuzi wa mitaani - na pia baada ya kushindwa kujikimu kupitia kilimo, Modou aliamua kujaribu kukaidi vikwazo vya kufika Ulaya kama mhamiaji haramu.
"Nilikuwa miongoni mwa waliokamatwa mwaka wa 2008 wakati mamlaka ilipopambana na wafanyabiashara wa mitaani waliokuwa wakifanya shughuli zao Marché Centenaire. Nilikaa gerezani kwa wiki moja kisha niliamua kuingia kwenye kilimo. Shukrani za pekee kwa binamu yangu ambaye ni mhandisi wa kilimo, niliweza kupata ujuzi katika nyanja hii, ambayo ninaipenda. Lakini ili kufanya kilimo, unahitaji rasilimali," anakumbuka Modou.
Mbali na changamoto ya kutafuta ardhi na ufadhili, pia kulikuwa na hali halisi ya soko ili kukabiliana nayo.
"Tulikuwa tumechukua mkopo wa milioni tatu kwa kuanzia. Lakini wakati wa mavuno, hatukuweza kuuza. Tuko katika nchi ambayo wakulima wadogo wanabanwa na wale wa kigeni. Wanasafirisha bidhaa zao kutoka nje ya nchi na kulijaza soko la Wasenegali uozo wao. Baada ya kutafakari kwa muda niligundua kuwa haifai kubaki bila shughuli. Hali ya nchi inatulazimisha kuchukua hatua na sio kuwa watazamaji tu. Kila unapoanza kuwa na matumaini, wanaishia kuharibu kila kitu. Kwa hiyo, ilitubidi kuondoka, kwa gharama yoyote ile,” anaiambia TRT Afrika.
Kufanya vibarua kuanzia Richard Toll hadi Nouakchott
Tofauti na wengi ambao hupanga safari yao kwa haraka kutokana na kukata tamaa kabisa, Modou aliamua kutoharakisha safari.
Lengo lilikuwa kufika Ulaya, lakini angejaribu kufikia mwisho wa safari hatua kwa hatua. Kijana huyo aliondoka Touba Toul ya asili yake kwanza kwenda kwa Richard Toll, kaskazini mwa Senegal.
Huko, alitumia mwezi mzima kuvuna mpunga na kuhifadhi pesa kabla ya kuanza tena safari yake.
"Nilipoondoka nyumbani, nilikuwa na takriban faranga 300,000. Nilikuwa na mpango madhubuti - kufanya safari kwa hatua na kufanya kazi njiani," anasimulia.
“Kuwasili kwangu Richard Toll kuliendana na msimu wa mavuno ya mpunga na nilifanya kazi kama kibarua wa msimu. Kutoka Richard Toll, nilivuka mto na kuingia Nouakchott, mji mkuu wa Mauritania. Bila kukawia, niliongeza safari yangu hadi Nouadhibou, kwa kuwa nilikuwa nimearifiwa kwamba ilikuwa rahisi zaidi kupata meli zilizokuwa zikielekea Hispania.”
Alipofika Nouadhibou, Modou aligundua kuwa hangeweza kupata ngalawa mara moja. "Niliamua kufanya kazi zisizo za kawaida ili kupata pesa. Baada ya kusubiri kwa muda mrefu bila kupata mtumbwi, niliamua kurudi Nouakchott. Huko pia, haikusaidia. Ndipo niliamua kuchukua njia ya ardhi kutoka Zouerate hadi Algeria, bila kujua kwamba huo ulikuwa mwanzo tu wa masaibu yetu,” asema.
Wakati Modou na wenzake walipoondoka Mauritania, wote walikuwa wamelipia safari ya kwenda Algeria. Lakini haikuwa hivyo. Baada ya saa nyingi njiani, yeye na kundi lingine walitupwa kilomita 30 kutoka mpaka wa Algeria, katikati ya jangwa.
Walikua hawajatambua, lakini huu ulikuwa mwanzo wa mapambano marefu, magumu vya kuishi katika uso wa mateso mengi.
"Tulikuwa na matumaini kwamba wakati huu tungefanikiwa. Lakini kwa mshangao wetu, wasafirishaji walituacha jangwani. Kulikuwa na askari walinzi kila mahali. Na ilitubidi tujilazimishe kupita njia kwa taabu kwa matumaini ya kujikuta tumefika Algeria. Ingawa tulifanikiwa, uchovu ulitufanya tuchukue mapumziko mafupi kabla ya kuendelea. Ilikuwa wakati huu ambapo walinzi walituzunguka. Huo ndio ulikuwa mwisho wa ndoto yetu, "Modou anakumbuka kwa kuangalia kwa mbali.
Mateso katika jangwa la Niger
Matumaini yoyote ya kufika Ulaya yalitoweka nchini Algeria. Mbaya zaidi njia ya vijana hawa kurudi nchini kwao ilionekana kufungwa. Wakilindwa kama ng'ombe, walitupwa jangwani kando ya mpaka wa Niger.
"Mara baada ya kukamatwa, wahamiaji hao wamekusanyika katika sehemu yenye ulinzi mkali, iliyoko Adrar. Kisha mamlaka hutengeneza msafara mkubwa. Kutoka Tamanrasset, wahamiaji hao hutupwa kwenye lori kama ng'ombe. Hali ni mbaya. Wakati msafara unaelekea jangwa la Niger, huna chaguo jingine ila kuendelea, ukitumai kupata kitu,” anasema Modou.
Wakiwa njiani kurejea katika nchi yao, Assamaka ilikuwa kituo cha kwanza cha wahamiaji waliokamatwa nchini Algeria. Hatimaye wangeishia Agadez, baada ya kipindi cha usafiri cha miezi mitatu hadi minne huko Arlit. Modou na marafiki zake hawana kumbukumbu zozote nzuri za vituo hivi.
"Katika eneo la Niger, tulipaswa kugundua aina nyingine ya changamoto. Huko Assamaka, Shirika la Kimataifa la Wahamiaji (IOM) linalofadhiliwa na Umoja wa Mataifa, ambalo huwajibika kuwarekebisha wahamiaji,’’ anasema Modou.
Pia anakumbuka aina ya dhuluma waliokabiliana nayo. ''Njia yao ni rahisi: kuishi kupitia migongo ya wahamiaji. Wanakusanya pesa kwa jina la uhamiaji, lakini hali ambayo wahamiaji wanaishi ni mbaya. Chakula sio kizuri na hakuna mtu anayeweza kulizungumzia. Kadiri tunavyokaa, ndivyo wanavyokusanya pesa nyingi. Mpaka ulipozuka uasi wa wahamiaji ndipo wakachukua uamuzi wa kuwapeleka Arlit. Vinginevyo mateso hudumu wastani wa mwezi, "anasema.
Kituo cha mwisho cha safari ya kurudi kilikuwa Agadez, ambapo wahamiaji hao wanaweza kuishia kukaa miezi miwili hadi minne kabla ya kurejeshwa nchini Senegal.
Kurudi kwenye uchungu kama mwanzo
Huku ndoto yake ya Euopean ikisambaratika, Modou alijitoa kurejea Touba Toul, mji wake wa asili, na kwa familia yake.
Kabla ya kuondoka kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Blaise Diagne huko Dakar, alikuwa amepokea, kama wenzake, uhakikisho kutoka kwa mamlaka ya Senegal. Hizi ni pamoja na ufadhili.
"Mamlaka iliweka ahadi ya kuwasaidia raia wanaojea nyumbani katika shughuli zao za kila siku. Hadi sasa, hakuna aliyesaidiwa. Hakuna aliyepata mafunzo au msaada," anasema.
Mchuuzi wa zamani wa barabarani bado ana majuto kwa kutofika Ulaya, haswa kwa vile wapo wachache waliofanikiwa.
"Jaribio langu la kwanza lilikuwa mwaka wa 2008. Najuta kutoendelea kama wengine. Sote tunaipenda nchi yetu, lakini hali ya leo haituruhusu kuwa na matumaini. Tuna familia, tuna wake na watoto. Lakini mamlaka yetu haitupi mbadala wa maisha. Mfadhaiko umeenea na tuna chaguzi mbili tu. Tunapaswa kufanikiwa na kutunza familia zetu au kufa na kuungana na wale ambao wametutangulia," asema.
Sasa ni baba wa watoto wawili, Modou lazima ajipange upya ili aione thamani yake katika jamii. “Nilijaribu kuanzisha ufugaji wa kuku. Hata nikawasilisha huo mradi kwa Serikali, lakini hadi sasa hakuna ufuatiliaji, wanakufanya ukimbie kutoka kushoto kwenda kulia, nakipenda kilimo na ni eneo ambalo naridhishwa nalo zaidi .
Kutoka kwa mgombea hadi ''wakili'' wa wahamiaji
Huko Touba Toul, maisha ya Modou yanahusu kazi ndogo ndogo ili kupata riziki. Anatumia muda wake wote katika kampeni dhidi ya uhamiaji haramu. Akifanya kazi kwenye mitandao ya kijamii, ambapo anajulikana kwa jina la Baye Fall Thiao, Modou's ni sauti ambayo hujishughulisha na watu kila mara na kuialika Serikali kuchukua hatua kukomesha janga la vijana kushindwa kuhamia nchi nyingine.
"Vijana hawachukui mitumbwi kwa starehe, wanaishi katika mazingira magumu, na hakuna kinachoweza kuwaondolea masaibu yao. Hawa ni vijana wanaoipenda nchi yao kwa dhati. Wanapojihatarisha ni kwa kusudi la kusaidia familia zao. Sisi ni raia na tuna haki ya kupata kazi zenye staha. Tunakaribisha Serikali kupeleka mikakati zake kukabiliana na janga hili. Nadhani inawezekana, kama kuna utashi," anasema Modou.
"Nilifanya majaribio mawili, na ningeweza kufia baharini au jangwani. Ni nafasi ya pekee kwangu kuwa bado hapa ili niweze kuzungumza juu ya mambo hayo. Hatupaswi kufumbia macho maigizo haya katika jamii," anaonya.
Akiwa amedhamiria kubeba sauti ya wahamiaji, Modou ameanzisha kikundi cha majadiliano kinachojumuisha wahamiaji waliorejeshwa nchini Senegal. Jukwaa linawaruhusu kuratibu shughuli zao na kuwasiliana na mashirika ya kiraia yanayofanya kazi katika masuala ya uhamiaji.
“Siyo rahisi kuanza tena baada ya kushindwa, hata katikati ya jamaa zako unachukuliwa kuwa mjinga, huna cha maana tofauti na waliojaribu na kufanikiwa kuingia ulaya. Kufadhaika ni jambo la kila siku na inaweza kukusukuma kwenye njia mbaya. Hivyo ni muhimu kuzungumza mara kwa mara na vijana," anasema.
Modou anaangazia hasa kujaribu kuwashawishi vijana wanaopanga kuondoka nchini wasikubali hatari zinazotokana nayo.
"Nina ushauri mmoja wa kuwapa vijana, ambao ni kuwataka wasijitoe mhanga. Kukaa hapa na kunyoosha mikono yetu sio suluhisho. Lakini nadhani kuruka kusikojulikana sio chaguo pia. Ni vigumu, lakini wajaribu kujijenga. Nina hakika kwamba ikiwa vijana wa Kiafrika watasimama imara, katika miaka mitano au sita, ni Wazungu ndio watakuja kuwatafuta na si vinginevyo."