Na Brian Okoth
Lucky Dube wa Afrika Kusini alikuwa kijana aliyekulia katika jimbo la mashariki la Mpumalanga mwanzoni mwa miaka ya 1980, hapo ndipo alipopata umaarufu, ambao ulimkuta akiwa tayari kuuteka ulimwengu.
Alizaliwa tarehe 3 Agosti 1964, Dube alilelewa na mamake alipokuwa mtoto mchanga. Baadaye, bibi yake alimchukua baada ya mama yake msanii huyo kwenda nje ya mji kutafuta kazi.
Wazazi wa mwanamuziki huyo walikuwa wametengana kabla ya kuzaliwa kwake. Dube alikuwa na ndugu wawili.
Shirika lisilo la kiserikali la African American Registry, limesema Dube alipewa jina la "Lucky" likiwa na maana bahati, na mama yake baada ya kupata mimba nyingi ambazo hazikufanikiwa.
Ndoto ya utotoni
Katika miaka yake ya mapema ya ujana, Dube alifanya kazi kama mtunza bustani, na baadaye alijiunga na shule akiwa na matumaini kwamba elimu ingemsaidia kupata kazi yenye malipo mazuri.
Ilikuwa katika siku zake shuleni ambapo alianzisha bendi iliyoitwa Skyway Band akiwa na marafiki zake wachache.
Katika miaka yake ya ujana, Dube alijiunga na bendi ya binamu yake iitwayo, The Love Brothers, iliyokuwa ikipiga muziki wa pop wa Kizulu uitwao Mbaqanga.
Hata hivyo aliondoka kwenye kundi hilo mwaka wa 1985, ili kutimiza ndoto yake ya utotoni ya kuwa msanii wa reggae. Albamu ya kwanza ya reggae ya Dube iitwayo "Rastas Never Die" ilitolewa mwaka huo.
Utambuzi wa kimataifa
Serikali ya Afrika Kusini hata hivyo iliipiga marufuku kutokana na maudhui iliyosema kuwa "ya kutatanisha."
Albamu za muziki za "Think About The Children" na "Slave", zilizofuata, zilipokelewa kwa furaha ndani na nje ya Afrika Kusini.
Kufikia 1987, Dube alikuwa mwanamuziki wa kwanza wa reggae wa Afrika Kusini kupata kutambuliwa kimataifa.
Watu wa kigezo katika safari zake za muziki, walikuwa wasanii wa reggae wa Jamaica Bob Marley, Jimmy Cliff, na Peter Tosh.
Kusajiliwa na Motown
Katika mahojiano, Dube alisema kuwa muziki wa reggae wa Jamaica ulikuwa na ujumbe wa kijamii na kisiasa ambao uliakisi kile kilichokuwa kikitokea Afrika Kusini wakati wa ubaguzi wa rangi.
Nyimbo "Prisoner", "House of Exile", miongoni mwa nyengine, zilimshindia tuzo nyingi mapema miaka ya 1990, na mnamo 1993, albamu yake iitwayo "Victims" iliuza nakala milioni moja ulimwenguni.
Kutokana na umaarufu wa kimataifa wa Dube, kampuni ya rekodi ya Marekani ya Motown ilimsajili katikati ya miaka ya 1990. Mwanamuziki huyo alisema amepata msukumo wa kuandika nyimbo kutoka kwa "mambo halisi yaliyotokea" karibu naye.
Wakati wa uchaguzi wa Afrika Kusini wa 1994, Dube alisema haijalishi ni rangi gani inatawala nchi hiyo mradi tu serikali inawakilisha watu wote.
Mauaji ya risasi
Mwanamuziki huyo ambaye alikuwa na zaidi ya albamu 20, alishinda tuzo kadhaa za kazi yake, ikiwa ni pamoja na Msanii Bora wa Kiafrika katika Tuzo za Muziki duniani.
Mnamo Oktoba 18, 2007, aliuawa kwa kupigwa risasi katika jiji la Johannesburg nchini Afrika Kusini katika kile kilichoripotiwa kuwa tukio la wizi wa gari.
Mnamo Aprili 2009, mahakama ya Johannesburg ilitoa hukumu ya kifungo cha maisha jela kwa wanaume watatu kwa kumpiga risasi msanii huyo.
Dube, ambaye alifariki akiwa na umri wa miaka 43, aliacha mke wake Zanele na watoto saba. Mnamo 2008, Afrika Kusini ilimtunuku Tuzo ya Mafanikio ya Maisha baada ya kifo chake.