Na Firmain Eric Mbadinga
Siku ya Magatte Ndiaye kwa kawaida huanza kwa mlo wa "Ndeki", au kifungua kinywa katika lugha ya Kiwolofu ya Senegali.
Ni utaratibu unaomwezesha kuvumulia mchana mzima kila siku kama dereva wa watu muhimu , VIP katika mji mkuu wa Senegal wa Dakar, mara nyingi bila mapumziko kwa chakula cha mchana.
Wiki nne zijazo ni tofauti. Sawa na Waislamu wengi wanaokadiriwa kufikia bilioni mbili duniani, Magatte amekuwa kwenye mfungo wa alfajiri hadi jioni tangu Machi 11, kuashiria mwanzo wa mwezi mtukufu wa Ramadhani.
Kama mtu yeyote aliyesoma au kukulia katika mila za Ramadhani anavyojua, kijana huyo anafahamu kwamba kula kabla ya jua macheo na baada ya jua kuzama katika kipindi hiki kunaleta faida nyingi za kiafya sambamba na kuweka hali ya nidhamu na kuimarisha imani ya kiroho.
Jinsi mwili unavyobadilika
Katika siku ya kwanza, mtu yeyote anayefunga kama Magatte yuko katika awamu ya mpito ya uzoefu wake wa kula. Udhibiti wa kimetaboliki ni kilele cha asili cha mabadiliko haya, ambayo hutoa faida zingine nyingi.
"Kufunga wakati wa Ramadhani hudhibiti sukari na homoni katika damu, hukusanya mafuta, na kutakasa mwili. Hukuza ufahamu wa lishe bora na ulaji wa afya kwa muda," mtaalamu wa lishe wa Senegal Jasmina Fall Ndour anaiambia TRT Afrika.
''Na bora zaidi , vijana hukabiliana na mabadiliko kwa haraka, na miili yao inakuwa na ufanisi zaidi katika kutumia nishati, ambayo yote yanaweza kusababisha faida za afya za muda mrefu."
Kwa watu wengine, changamoto kutoka kwa mtazamo wa kisaikolojia ni udumishaji kwa makini mabadiliko haya ya lishe.
"Jambo kuu la kufanya ni kufuata lishe yenye afya, yaani, kuepuka, kama tunavyosema siku zote, chochote kilicho na sukari nyingi, chumvi na mafuta. Pia, mtu anahitaji kujumuisha virutubisho muhimu katika chakula; " Jasmina anashauri.
Kama moja ya nguzo tano za Uislamu, kufunga wakati wa Ramadhani ni tofauti na kujizuia kawaida na chakula kwa muda maalum kwa sababu nyingine. Kushikamana na utamaduni huu ni, juu ya yote, kitendo cha imani na utii kila Mwislamu lazima atekeleze kwa wajibu, isipokuwa kwa wachache wanaoruhusiwa kutofunga.
Usimamizi wa kimwili
Jambo la kushangaza zaidi ni jinsi sheria za mfungo wa Ramadhani zinavyolingana na mapendekezo ya madaktari wa kawaida.
"Katika suala la iwapo kila mtu anaweza kushika mfungo wa Ramadhani, ifahamike kuwa madhara ya mfungo yanaweza kutofautiana kutoka kwa mtu mmoja hadi mwingine, kutegemeana na mambo kama vile umri na afya kwa ujumla," mtaalamu wa lishe Jasmina anaiambia TRT Afrika.
Kwa hivyo, ikiwa hakuna sababu ya kiafya ya kumzuia mtu dhidi ya kukosa chakula kuanzia alfajiri hadi jioni, funga ya Ramadhani inaweza kuwa na manufaa makubwa kwa kila mtu.
Kwa watu wanaoweza kufunga, inashauriwa kusimamia miili na juhudi zao, haswa mwanzoni mwa mfungo. Shughuli za michezo zinazohitaji nishati nyingi hazipendekezi wakati huu.
Magatte, mwanasoka mahiri ambaye anacheza mchezo huo kama hobby, anachukua likizo ya mwezi mmoja ili kuepuka kuudhoofisha mwili wake wa kufunga.
"Pia unahitaji kuhakikisha kuwa unakunywa maji ya ya kutosha wakati wa saa unazoruhusiwa. Pia, epuka shughuli zozote za kimwili ambazo ni kali sana, kwa usahihi ili kuepuka athari na mabadiliko makubwa ya kisaikolojia," anasema Jasmina.
Hatari za kula kupita kiasi
Wataalamu wa lishe wanapendekeza kujizuia na nidhamu kwa wale wanaojaribiwa na hamu ya kula na kunywa kila kitu haraka baada ya kumalizika saa za mfungo.
"Siyo jambo la ajabu kuona watu wanakula kupita kiasi kwa haraka haraka. Hapa Senegal, hilo linaonekana kuwa tatizo," anasema Jasmina.
"Mwisho wa mfungo wa siku, kuchagua vyakula vinavyorejesha nishati, kurejesha maji mwilini na kutupatia virutubishi muhimu ni muhimu. Ni vyema kuanza taratibu na tende, maji kidogo au chai ya mitishamba na supu nyepesi. Zipe kipaumbele matunda badala ya chakula kingi."
Jambo kuu ni kuchukua muda kula badala ya kubugia haraka haraka. "Kwa nini usitumie nyakati za maombi kama mapumziko?" anapendekeza mtaalamu wa lishe.
Kwa mujibu wa mtaalamu huyo wa masuala ya lishe, mkazo usiwe kwenye idadi ya milo au kiasi kinacholiwa bali ubora wa chakula.
"Jambo muhimu zaidi kukumbuka ni kuepuka kula milo mikubwa. Hiyo ndiyo taarifa muhimu zaidi. Unapaswa kutanguliza usawa wa milo midogo midogo, miwili au mitatu, mradi tu iwe imekamilika," anasema.
Kufunga katika Uislamu sio tu kujizuia kula na kunywa, pia kunahusisha kutojamiiana wakati wa saumu.
Waislamu pia wanatakiwa kujitolea muda zaidi kusoma Quran na kuswali swala za usiku.