Dayo Yusuf
TRT Afrika, Istanbul, Uturuki
Ramadhani ina raha yake ambayo wengi wanaiangalia kwa hamu sana. Mojawapo ni futari.
Yaani inapofika magharibi wakati wa kufungua swaumu, maakulati na mapochopocho ya kila aina yanaandaliwa. Kawaida uswahilini jamvi linakuwa limeandaliwa na wote wanakaa mkao wa kula.
Utakuta vitu kama kaimati, katlesi, mahamri au maandazi, matobosha, tambi za kila aina, mikate, yani utashindwa mwenyewe.
Lakini umewahi kujiuliza vyakula unavyovikuta au unavyopendelea kula wakati huo vina manufaa gani kwako?
Wataalamu wanashauri wakati wote uzingatie lishe bora yenye virutubisho vya kutosha. Lakini wakati wa mfungo ndio unatakiwa kuwa muangalifu zaidi ili usije kudhoofisha afya yako.
Wizara ya Afya ya Uturuki ilitoa muelekezo mwaka jana wa namna ya kuimarisha lishe bora na kutunza afya yako wakati wa Ramadhan kupitia vyakula.
Mwanzo wanashauri, ukiwa unafunga, usikose kula daku, yaani kile chakula cha mapema alfajiri kabla ya kuanza kufunga.
Hata kama ni tende na maziwa au chakula cha laini, kisha unywe maji. Inapofika wakati wa Iftar unashauriwa uanze kwa supu na saladi.
Kula kiasi kidogo kidogo kwa kugawa badala ya kula chakula kingi kwa wakati mmoja. Pika chakula kwa njia bora kama vile kuchemsha au kuoka.
Epuka vyakula vya kuchoma, kukaanga kwa mafuta mengi, au vya moshi. Kunywa maji mengi baada ya kufuturu kuzuia kuishiwa na maji mwilini.
Ukipata matunda freshi, au yaliyokaushwa, karanga, maziwa yawe ya freshi au ya mtindi ni bora baada ya iftar.
Weka umuhimu kwa vyakula vilivyo na vitamin A, C, D na E ambavyo vinaimarisha kinga mwilini.
Wakati mwengine unakuta wazazi wanapika vyakula vinavyolenga kuwavutia watoto kula kwa kuwaonea huruma kuwa wamefunga mchana kutwa.
Hapo ndipo kosa linapotokea kwa sababu kumlisha mtoto vitu vitamu pekee zinaweza kumdhuru.
Pia kitu chengine ambacho kinaweza kushawishi aina ya chakula kitakachopikwa ni pamoja na gharama, kutokana na hali ngumu ya uchumi.
Na usisahau, kwa kuwa umefunga, haina maana kuwa ndio kulala tu mchana kutwa, jitengee muda kidogo wa mazoezi japo kwa mepesi.