Abuja ilikuwa miongoni mwa maeneo ambayo uporaji na uchomaji ulifanyika wakati wa maandamano dhidi ya gharama ya maisha. Picha: Reuters

Na

Abdulwasiu Hassan

Ibrahim Garba Wala hawezi kustahimili mshtuko wa kuona mradi wa biashara ambao ulichukua miaka ya uvumilivu na taabu kuujenga ukiharibiwa katika dakika chache za ghadhabu ya umati isiyoweza kupunguzwa.

Mjasiriamali huyo anayeishi Kano, ambaye anamiliki kampuni mtandaoni za ShawaliNG.com na FundME, si mfanyabiashara pekee anayehesabu hasara zake, huku Nigeria ikikabiliana na ongezeko la machafuko barabarani kutokana na mfumuko mkubwa wa bei uliochochewa na kuondolewa kwa ruzuku ya mafuta.

"Tulipoteza kila kitu tulichokuwa nacho katika jengo ambalo ni makao makuu yetu," Wala anaiambia TRT Afrika.

"Samani, kompyuta, friji, mashine ya kupasha moto chakula 'microwaves', mashini ya maji baridi na moto 'dispenser', nyaraka - kila kitu kiliibiwa au kuharibiwa. Hata madirisha na milango iling'olewa."

Maandamano hayo yalikusudiwa kuvuta hisia za serikali kuhusu jinsi kupanda kwa gharama ya maisha ilivyokuwa ikiathiri kaya katika nchi hiyo yenye watu wengi zaidi barani Afrika.

Badala yake, maandamano hayo yaligeuka haraka na kuwa uporaji uliohusisha makundi ya watu waliokuwa wakiishambulia serikali na taasisi za kibinafsi.

Katika hotuba kwa Wanigeria, Rais Bola Tinubu alitoa wito wa kusitishwa kwa maandamano hayo, akisema serikali imezingatia malalamiko ya wananchi.

Maandamano hayo yalianza Agosti 1 huku raia wa Nigeria wakidai kupunguzwa kwa gharama za maisha. Picha: Reuters

“Maandamano hayo ambayo yaligeuka kuwa ya vurugu katika baadhi ya maeneo ya taifa letu, yamesababisha maumivu na hasara isiyoelezeka, hasa kwa familia za watu waliopoteza maisha kwa njia ya kusikitisha,” alisema. "Rasilimali za taifa letu ni kidogo sana ikijiwa suala la kujenga upya kile ambacho kimeharibiwa."

Uharibifu wa aibu

Kiwanda kipya cha Kidijitali katika Jimbo la Kano, kiliyobuniwa na serikali kama kitovu cha uvumbuzi, kujenga uwezo wa kibiashara kwa biashara za kizazi kipya, pia kilishambuliwa na makundi ya watu.

Kuonekana kwa waharibifu wakibeba kompyuta na vifaa vilivyokusudiwa kujenga ujuzi wa kidijitali kuliashiria ukubwa wa uporaji.

"Inasikitisha kujua kwamba Kiwanda chetu cha Ubunifu wa Kidijitali huko Kano kinachotarajiwa kuzinduliwa wiki ijayo ili kusaidia kiongeza kasi cha talanta ya kiufundi (3MTT) kimechomwa moto na kuporwa na waandamanaji," waziri wa mawasiliano, uvumbuzi na uchumi wa kidijitali wa Nigeria aliandika kwenye mtandao wa kijamii wa X tarehe 1 Agosti.

Biashara kama vile Barakat Stores, duka kuu la kihistoria huko Kano ambalo lililengwa na umati wa watu, wanasema uharibifu wa uchumi utafikia mabilioni ya pesa zaidi kuliko ilivyokadiriwa hapo awali.

"Tunatafuta msaada wa Mungu na serikali ili kukabiliana na hili," mwakilishi wa Barakat anaiambia TRT Afrika.

Wala bado anajaribu kufanya makadirio ya kina ya thamani ya samani, kompyuta, vifaa vya elektroniki na vitu vingine vilivyoharibiwa au kuporwa. Bima ilithamini jumla ya mali kuwa zaidi ya naira milioni 75.

Upungufu wa ajira

Watu wengi wanaofanya kazi katika mashirika ya kibinafsi yaliyoporwa wamepoteza riziki zao.

"Sehemu inayosumbua zaidi ya kile ambacho kimetokea tangu mwanzoni mwa Agosti ni idadi ya familia ambazo zimepoteza chanzo chao cha mapato. Unawezaje kuendeleza kazi ikiwa biashara haiwezi kuendelea?" Wala anaiambia TRT Afrika.

Mjasiriamali huyo ameajiri wafanyikazi 30 na zaidi ya mawakala 100 huko Kano na majimbo mengine yaliyoathiriwa.

Maduka ya Barakat imelazimika kupoteza wafanyakazi kwa sababu ya hasara kubwa.

"Kabla ya wimbi la uporaji, zaidi ya watu 300 walikuwa wakipata riziki kupitia duka hilo," anasema afisa wa Barakat Stores.

"Watu wengi wanaenda kwenye soko la ajira kwani hawana tena kazi za kawaida."

Hofu ya kuwekeza tena

Wafanyabiashara ambao wamepata hasara kubwa wa uporaji tangu ghasia kuanza wanahofia kuwekeza pesa ili kuzifufua kwa sababu ya kutokuwa na uhakika.

"Kusema kweli, nimepoteza imani katika kuwekeza Kano au sehemu nyingine yoyote nchini Nigeria kwa sababu ya hiyo," Wala anaiambia TRT Afrika.

Wamiliki wa Barakat Stores wana maoni haya, ingawa yao ni biashara ya jadi iliyokita Kano.

"Kila kinapotokea kisa kama hiki, kitazuia watu kujitokeza kuwekeza, kuzindua biashara na kutengeneza ajira. Hatimaye, jimbo litaendelea kuwa na maendeleo duni, na kutakuwa na watu wengi wasio na kazi karibu na kukosekana kwa kazi," afisa mmjoa anasema.

Wala anakusudia kubadilisha mkakati wake ikiwa na kama ataamua kuwekeza tena.

"Nitaepuka majimbo ambayo ni hatarishi kiusalama. Ninafikiria hata kuhamisha biashara zangu nje ya nchi kwa sasa ili tuweze kuendesha shughuli kwa mbali na labda ushirikiano wa mbali na washirika wa ndani," anaelezea.

Vyovyote vile, wamiliki wa biashara wanatumai serikali italinda mazingira ya kiuchumi na kujiandaa vyema kwa usumbufu unaoweza kutokea.

"Ni muhimu kwa serikali kuhakikisha kuwa popote palipo na biashara, wanahitaji kulindwa. Kwa nini wasubiri wafanyabiashara waombe usalama? Hiyo inapaswa kutolewa," anasema Wala.

TRT Afrika