Vita Sudan vimelazimisha zaidi ya watu milioni mbili kutoroka makwao/ Picha: Reuters

Kamanda wa Kikosi cha Msaada wa haraka, Rapid Support Forces (RSF) alitangaza usitishaji mapigano wa siku mbili unaoanza Jumanne ili kuzingatia sikukuu ya waislamu ya Eid al-Adha.

"Tunatangaza kusitisha mapigano kwa upande mmoja, huku tukiwa kwa hali ya kujilinda, mkesha wa Eid na siku ya Eid al-Adha," Mohammad Hamdan Dagalo, anayejulikana pia kama Hemedti, alisema Jumatatu katika rekodi ya sauti iliyowekwa kwenye Facebook.

Hata hivyo Wanajeshi wa Sudan wameuita wito wa kundi la wanamgambo wa kusitisha mapigano wakati wa Eid Al-Adha kwa ujanja tu.

Katika taarifa ambayo TRT Afrika imeona, Brigedia Jenerali Al-Tahir Abu Haja wa jeshi la Sudan alisema: "Ni mbinu ya RSF kujisafishia jina baada ya uhalifu wa kutisha iliyofanya dhidi ya raia."

Dagalo alielezea matumaini kuwa sikukuu ya Eid itatoa fursa ya maridhiano kati ya watu wa Sudan.

Akikubali changamoto za hali ya kibinadamu iliyosababishwa na vita, alisema:

Tunatumai kuibuka kutoka kwa vita tukiwa na umoja na nguvu zaidi." Eid al-Adha, au Sikukuu ya Sadaka, ni moja ya sikukuu muhimu zaidi za Waislamu, inayoashiria kilele cha hija ya kila mwaka nchini Saudi Arabia.

Sudan imekumbwa na mapigano kati ya jeshi na RSF tangu katikati ya mwezi wa Aprili katika mzozo ulioua karibu raia 1,000 na kujeruhi wengine 5,000, kulingana na takwimu ya madakitari.

Shirika la Kimataifa la Uhamiaji (IOM) linakadiria kuwa mzozo huo umesababisha zaidi ya watu milioni 2.2 kuyahama makazi yao.

Mipango kadhaa ya kusitisha mapigano ilitangazwa katika kipindi kilichopita.

Hata hivyo pande zinazozozana zilishutumu kila mmoja kwa kukiuka makubaliano ya kusitisha mapigano.

"

TRT Afrika na mashirika ya habari