Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Muliro J Muliro./Picha: Wengine

Jeshi la Polisi Kanda Maalumu Dar es Salaam linamshikilia Derick Derick Junior kwa tuhuma za kujeruhi na kutishia watu kwa silaha.

Kulingana na taarifa iliyotolewa na Muliro J Muliro, ambaye ni Kamanda wa Kanda Maalumu ya Polisi Dar es Salaam, tukio hilo lilitokea Oktoba 27, 2024 kwenye sehemu ya burudani iitwayo ‘1245 night club’ katika eneo la Kinondoni, ambapo mtuhumiwa alimjeruhi Julian Bujuru kwa kumpiga na kitako cha bastola na kumsababishia majeraha katika sehemu za jicho na pua.

Picha mjongeo ambazo zilianza kuonekana kwenye mitandao ya kijamii mapema Oktoba 28, zilimuonesha mwanaume mmoja akitishia watu kwa silaha.

“Kitendo hicho hakikubaliki na ni kinyume na sheria…aliyejeruhiwa anaendelea vizuri na matibabu,” alisema Muliro.

Kamanda huyo wa Polisi, pia aliongeza kuwa Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na Ofisi ya Taifa Mashtaka linakamilisha utaratibu wa kisheria ili mtuhumiwa aweze kufikishwa katika vyombo vingine vya sheria, haraka iwezekanavyo.

“Jeshi la Polisi linatoa wito kwa wananchi kuwa halitosita kumchukulia hatua mtu yeyote anayemiliki silaha, atakayebainika kufanya matendo ambayo ni kinyume na sheria, kanuni na taratibu zilizoainishwa katika kibali chake cha kumiliki silaha,” Muliro aliongeza.

TRT Afrika