Makamu wa Rais wa Tanzania Dkt Philip Mpango, amelitaka Jeshi la Polisi la nchi hiyo kuanza kutumia majaketi maalumu yaliyofungwa kamera maalumu ili kuchunguza mienendo ya polisi wa usalama barabarani, wawapo kwenye majukumu yao.
Dkt Mpango, ambaye alikuwa anazungumza siku ya Mei 11, 2024, katika mji mkuu wa nchi hiyo Dodoma, alisisitiza umuhimu wa teknolojia katika kudhibiti rushwa barabarani.
"Nimeliagiza Jeshi la Polisi kupitia upya mchakato wa utoaji wa leseni za uendeshaji wa magari na ukaguzi wa magari hayo. Vile vile, tunalenga kufunga kamera maalumu barabarani na kwenye nguo za maofisa wa usalama barabarani ili kudhibiti rushwa na kuongeza ufanisi," amesema Dkt Mpango.
Makamu huyo wa Rais, ameweka wazi kuwa amemshirikisha Waziri wa Mambo ya Ndani wa nchi hiyo Hamad Masauni, namna ya kuanza utekelezwaji wa mkakati huo.