Serikali ya Italy imesema kuwa itairejeshea Ethiopia ndege yake, ijulikanayo kama "Tsehay".
" Ndege hii yenye viti viwili ni ya kwanza kutengenezwa nchini Ethiopia mnamo mwaka 1935 kwa ushirikiano wa wananchi na Herr Ludwig Weber," waziri mkuu wa Ethiopia, Abiy Ahmed ameelezea katika ukurasa wake wa X.
Jina lake lilichaguliwa kwa heshima ya malkia Tsehay, binti ya Mtawala wa wakati huo Haile Selassie.
"Leo ni siku ya fahari kubwa kwa Waethiopia tunaposherehekea makabidhiano rasmi ya "Tsehay" kutoka serikali ya Italy. Natoa shukrani zangu nyingi kwa Waziri Mkuu Giorgia Meloni kwa hatua yake ya kuwezesha kurejeshwa kwa ndege hii,” alisema Abiy baada ya kuipokea ndege hiyo huko Italy.
Kulingana na wataalamu wa historia, ndege hiyo ilipelekwa Italy baada ya majeshi vamizi yaliyoongozwa na dikteta Benito Mussolini kuiteka Ethiopia, kisha Abyssinia, mwaka wa 1935, na kuchukua mji mkuu Addis Ababa mwaka uliofuata.
Wizara ya Ulinzi ya Italy ilisema ndege hiyo ya viti viwili, ambayo awali ilikuwa na rangi ya kijivu na fedha, lakini sasa imepakwa rangi nyekundu, iliruka kwa mara ya kwanza mnamo Desemba 1935.
Chombo hicho cha usafiri kilitumia saa 30 angani na kisha kutelekezwa huko Addis Ababa, Mei 1936, kabla ya kuwasili kwa Waitaliano, ambao waliiomba," ilisema sehemu ya taarifa ya wanahistoria hao.
Wizara hiyo ilisema ndege hiyo, iliyokuwa imehifadhiwa katika makumbusho ya jeshi la anga la Italy tangu 1941 na baadaye itasafirishwa hadi Ethiopia katika maonyesho maalumu.
Hata hivyo, taarifa za kusafirishwa kwa ndege hiyo bado hazijawekwa wazi.
Serikali ya Ethiopia inasema “Tsehay" ndiyo ndege pekee iliyotengenezwa nchini Ethiopia kabla ya Vita vya Pili vya Dunia. Ndege hiyo ilitengenezwa kwa rasilimali chache, ikitumia zaidi mafundi seremala wa kipindi hicho.