Takriban watu 843,130 wamelazimika kuwa wakimbizi wa ndani tangu kuanza kwa machafuko nchini Sudan, shirika la kimataifa la uhamiaji, IOM, limesema.
IOM imetoa onyo Jumatano kuwa zaidi ya watu 1.8 milioni wanatarajiwa kupoteza makwao iwapo ghasia hizo zitaendelea.
Pia shirika hilo lilisema kuwa tayari kulikuwa na wakimbizi wapatao milioni 1.1 na wengine 3.8 milioni waliopoteza makwao nchini humo kabla ya vita hivyo kuanza.
Ilisema kuwa huku watu zaidi ya 259,000 wakiwa wamekimbilia nchi jirani, kuna hofu ya wakimbizi zaidi ya milioni moja na wahamiaji nchini humo watakao athirika iwapo ghasia zitaendelea.
Kwa mujibu wa shirika hilo, msaada wa kibinadamu unahitajika kwa dharura kwa watu wapatao milioni 25.7 ndani na nje ya Sudan.
Msaada huo unalenga kukidhi mahitaji ya $105 milioni kwa watu wa Sudan, $104 milioni nchini Misri, Libya, Chad, Jamhuri ya Afrika ya Kati, Sudan ya Kusini na Ethiopia.
"Hali iliyoko sasa Sudan ndio mbaya zaidi iliyowahi kutokea nchini humo," Mkurugenzi Mkuu wa IOM Antonio Vitorino alisema katika taarifa.
"Mamilioni wanakosa mahitaji ya kimsingi kama vile maji, chakula na makao. Tusipowajibika sasa, wananchi wa Sudan watakumbwa na janga kubwa na mbaya sana,’’ amesema Vitorino.
"Tunatoa wito kwa jamii ya kimataifa kuchangia kwa dharura juhudi za msaada kwa kukusanya fedha zinaohitajika kukabili mahitaji."