Na Coletta Wanjohi
Istanbul, Uturuki
Sudan Kusini Na uchaguzi Wananchi wa Sudan Kusini walikuwa wamejitayarisha kupiga kura kwa mara ya kwanza Desemba 22 mwaka huu , tangu nchi hiyo kupata uhuru mwaka 2011.
Lakini sasa itabidi wasubiri , kwani serikali yao imehairisha uchaguzi mkuu hadi 2026. Hii ni mara ya pili kwa uchaguzi mkuu kuhairishwa nchini humo baada ya uongozi wa mpito kuanza Februari 2020.
Baada ya vita kuzuka Desemba 2013 kati ya serikali ya Rais Salva Kiir na makamu wake wa wakati huo Riek Machar , nchi hiyo ilitoswa katika changamoto kubwa ambayo hadi leo, miaka 11 baadaye, wanakumbwa na athari zake.
Zaidi ya watu 400,000 wanaripotiwa walikufa na mamilioni kulazimia kuhama makazi yao , wengine wakikimbilia nchi jirani kwa usalama.
Makubaliano ya amani ya 2018 yalistisha vita hivyo ikiwa na lengo kuu la kuandaa uchaguzi mkuu na kuwapa fursa wananchi wa Sudan kusini kuchagua viongozi wao .
Lakini ina maana gani kwa Sudan Kusini kukosa kufanya uchaguzi mwaka huu?
Tayari umoja wa mataifa na Tume ya kufuatilia utimizaji wa makubaliano ya amani nchini Sudan kuisni zilikuwa zimesema mara kwa mara kuwa nchi hiyo haiko tayari kwa uchaguzi.
Inaamisha kuwa viongozi waliozozaza na vita kuzuka Desemba 2013 wataendelea kushikilia uongozi wa nchi hiyo kwa pamoja kwa miaka miwili ijayo , huku serikali ya mpito ikiendelea kuongozwa na Rais Salva Kiir.
Muda zaidi utaipa nchi hiyo nafasi ya kutimiza mfumo wa kuwaingiza waliokuwa wanajeshi wa waasi ndani ya jeshi la taifa.
Takriban wanajeshi 55,000 kati ya 83,000 wa awamu ya Umoja wa Wanajeshi wameshapewa mafunzo na kufuzu.
Maafisa wa polisi 2,995 wameingizwa katika kikosi cha polisi na kupewa majukumu. Sudan Kusini sasa ina muda wa kuunda katiba ya kudumu, na kutimiza vipengele vyote vya tume ya uchaguzi.
Baraza la Vyama vya Siasa limepitisha Kanuni ya Maadili, na kusajili vyama vya siasa 29, lakini kuna wasiwasi kuhusu taratibu zinazofuatwa, na ada za usajili.
Tume ya Kitaifa ya Uchaguzi imeunda upya Kamati Kuu za ngazi ya Majimbo, lakini kuna wasiwasi kuhusu vigezo vinavyotumika, na uwakilishi wa jinsia. Sasa kuna wakati wa kutatua haya yote.
Sudan Kusini imepitisha sheria mbili za kutetea haki za walioathiriwa na vita tangu 2013, sasa ina nafasi ya kuzichambua na labda kuwapa haki watu kabla ya uchaguzi ujao.
Pia kuna muda wa Umoja wa Afrika kutimiza jukumu la kusaidia Sudan Kusini kuunda mahakama ya mseto yaani Hybrid Court ambayo itakuwa na mamlaka ya kuchunguza na kuwafungulia mashtaka watu wanaohusika na uhalifu mkubwa uliofanywa tangu tarehe 15 Disemba 2013 nchini humo.
Serikali ya Sudan Kusini imesema muda zaidi itaipa wakati wa kutafuta rasiliamli inayotosha kuandaa uchaguzi mkuu.
Na huku wananchi wengine wa Sudan Kusini wakiunga mkono kuhairishwa kwa uchaguzi huu , wengine hawajafurahia kwani wanasema maendeleo ya uchumi na kijamii ya Sudan Kusini bado yanabaki kwa serikali ya mpito ambayo imeundwa na washikadau wale wale walioifanya nchi hiyo kuingia vitani 2013.
Swali ni Sudan Kusini itakuwa tayari kwa uchaguzi mwaka 2026?