Msemaji wa shirika la Umoja wa Mataifa la watoto UNICEF, ameelezea wasiwasi kuwa asilimia 90 ya wakimbizi hao ni mama na watoto ambao wengi wao wana wasili wameathiriwa na utapia mlo.
Msemaji Olga Sarrado ameambia waandishi wa habari mjini Geneva kuwa zaidi ya watu 30,000, wamewasili katika siku chache zilizopita.
Idadi kubwa ya wanaokimbia mapigano hayo wanapitia njia hatari ikiwemo njia za jangwani kuelekea Chad.
UNHCR imetoa wito wa ufadhili wa dharura kwa mashirika yote yanayohusika na kuwaokoa wakimbizi au kuwapokea ili kuepuka janga la kibinadamu linalotishia kutokana na hali inavyo endelea kuzorota.
"Misaada imekuwa ikichelewa hasa kutoka kwa sekta ya kibifasi ikilinganishwa na mashirika mengine mikubwa, licha ya hali ya dharura iliyopo,’’ aliongeza.
Wiki iliyopita, shirika hilo lilitoa wito wa ufadhili wa takriban dola milioni 445, ambapo wito mpya huu ni kuongezea kwa idadi hiyo.
Wakati huo huo, Umoja wa mataifa umesema kuwa kampuni moja ya kutengeneza chakula cha watoto walioathiriwa na utapia mlo, limechomwa moto. Msemaji wa UN, amenukuliwa katika mtandao wa shirika la habari la Reuters kusema kuwa haijulikani nani aliyehusika na tendo hilo.
Kwingineko muungano wa mashirika matatu yaani Umoja wa Afrika, AU, Umoja wa Mataifa na shirika la IGAD, UNITAM, umepongeza hatua ya kusainiwa makubaliano ya kuruhusu kupitishwa misaada na kuwalinda raia nchini Sudan.
Makubaliano hayo yalitiwa saini kati ya jeshi la Sudan, na kikosi cha dharura cha RSF, wanaokutana mjini Jeddah, Saudi Arabia.
Mashirika haya yamewataka viongozi wa vikosi hivyo kuwasilisha ujumbe kwa wapiganaji wao walioko nchini Sudan na kufuatilia kuhakikisha wanatekeleza.
Mashirika hayo yametoa wito kwa makundi yanayopigana kuwa wanapoendelea na mazungumzo, watilie maanani umuhimu wa kuwashirikisha raia na wadau wa kisiasa, wakiwemo wanawake.
‘’Hii ni hatua muhimu katika kuwapunguzia mateso raia wa Sudan na kulinda maisha na hadhi yao wakati huu mgumu’’ shirika hilo liliongezea.