Raia wa Palestina wakiomboleza kifo cha mpendwa wao katika Hospitali ya Nasser huku mashambulizi ya Israeli yakiendelea katika eneo la Khan Younis, Gaza Disemba 17, 2023. / Picha: Maktaba AA  / Photo: AA Archive

Israeli inatumia mbinu ya njaa kama “silaha ya kivita” Gaza kwa makusudi wakiwakatia watu huduma muhimu za maji na chakula, ambayo ni uhalifu wa kivita, Shirika la Human Rights Watch (HRW) limesema.

“Vikosi vya Israeli kwa makusudi vimezuia usambazaji wa maji, chakula, na mafuta, huku wakisambaratisha msaada wa kibinadamu, na kuharibu maeneo ya kilimo, na kuwanyima wananchi huduma muhimu za kuwasaidia kuishi,” limesema Shirika hilo katika taarifa yake.

Imeonyesha kauli iliyotolewa na viongozi wakuu wa Israeli, akiwemo Waziri wa Ulinzi Yoav Gallant, Waziri wa Ulinzi wa Taifa Itamar Ben-Gvir, na Waziri wa Nishati Israel Katz kuhusu nia yao ya “kuwanyima chakula wakazi wa Gaza, maji na mafuta – kauli zinazoonyesha sera inayoendeshwa na vikosi vya Israeli.”

Maafisa wengine wa Israeli, imeongeza taarifa hiyo, wamesema wazi wazi kwamba msaada wa kibinadamu Gaza aidha utaambatana na masharti ya kuachiliwa kwa mateka wanaoshikiliwa na Hamas kinyume cha sheria.

“Kwa zaidi ya miezi miwili sasa, Israeli imekuwa ikiwanyima wakazi wa Gaza chakula na maji, sera ambayo inaendeshwa na maafisa wa ngazi ya juu wa Israeli na inaonyesha nia yao ya kuwanyima chakula kama silaha ya kivita,” amesema Omar Shakir, mkurugenzi wa HRW tawi la IsraelI na Palestina.

“Viongozi wa dunia sharti wazungumze dhidi ya uhalifu huu, ambao una athari kubwa kwa wakazi wa Gaza."

HRW imesema sheria za dunia za kibinadamu, au sheria za vita, zinakataza kuwanyima raia chakula kama njama ya vita.

Mashambulizi ya Israeli ya anga na ardhini dhidi ya Gaza tangu shambulio la Hamas la Oktoba 7 yameua zaidi ya raia wa Palestina 18,700, wengi wao wanawake na watoto, na kujeruhi wengi.

Vita hivyo, vimeiacha Gaza ikiwa na uharibifu mkubwa huku nusu ya nyumba zikiwa zimeharibiwa, na takriban watu milioni mbili wameachwa bila makazi katika eneo linalokaliwa na wengi huku kukiwa na ukosefu wa chakula.

TRT World