Zaidi ya watu milioni sita walilazimika kuyahama makazi yao ndani / Picha: Reuters

Na Coletta Wanjohi

TRT Afrika, Istanbul, Uturuki

Tangu Aprili 15, 2024, Antasar Jouma Adam hajawa na amani. Vita kati ya vikosi vya Wanajeshi wa Sudan na wanamgambo wa kundi la Rapid Support Forces, RSF, vilivyoanza 15 Aprili 2023 vimeleta madhara tupu.

"Wapwa na shangazi zangu na zaidi ya watu 15 au 16 wa familia yangu wamepotea, na hatujui kinachoendelea kuhusu hali yao," alisema Antasar Jouma Adam, ambaye alikimbia nyumbani kwake mwanzoni mwa mzozo na kupata sehemu ya kuishi mjini Port Sudan.

Ansara ni kati ya zaidi ya watu milioni sita waliolazimika kuyahama makazi yao.

Umoja wa Mataifa (UN) unasema kuwa takriban wakimbizi milioni mbili wamekimbilia nchi jirani za Chad, Sudan Kusini, Ethiopia na Misri.

Takriban watu milioni 24 wanahitaji msaada, huku milioni 18 wakiteseka kwa viwango vya uhaba wa chakula, kulingana na UN.

Wajdan Hassan Ahmed, muuguzi wa Shirika la Sudanese Red Crescent Society (SRCS) ni raia wa Sudan na bado anawahudumia raia wenzake/ picha kutoka ICRC

Antsar anategemea usaidiza kambini kutoka kwa mashirika kama Kamati ya Kimataifa ya Msalaba Mwekundu (ICRC) na watu wa kujitolea kutoka Jumuiya ya Hilali Nyekundu ya Sudan (SRCS).

Lakini wahudumu pia ambao ni raia wa Sudan hawana afueni ya aina yoyote.

Wajdan Hassan Ahmed, muuguzi wa SRCS kwa zaidi ya miaka 15, anakumbuka hali mbaya ambayo mamilioni ya watu nchini Sudan tayari wamepitia.

"Mwaka wa vita umekuwa mgumu zaidi, niliishi kama raia na pia mfanyakazi wa kujitolea nchini Sudan, " anaelezea Wajdan.

"Miongoni mwa nyakati ngumu sana zilikuwa kuhamishwa kwa watu ambao walikuwa wameharibiwa na vipande vya bomu, hadithi za baba waliopoteza binti zao, mama waliopoteza watoto wao, wazazi ambao walipoteza wanafamilia wao wote," aliongeza.

Zaidi ya watu 700,000 kutoka sudanw amekimbiali nchi jirani ya Chad/ Picha kutoka Norwegian Refugee Council

Hali ya kibinadamu inazorota

Baraza la Haki za Kibinadamu lilianzisha Ujumbe wa kufanya utafiti nchini Sudan mwezi Oktoba 2023. Moja ya kazi zake kuu ni kuchunguza na kubaini ukweli, mazingira na sababu za msingi za ukiukwaji wote wa haki za kibinadamu na ukiukwaji wa sheria za kimataifa za kibinadamu.

"Pande zinazopigana Sudan zina wajibu wa kisheria kulinda raia, lakini zimeonyesha kutojali kufanya hivyo," Mohamed Chande Othman mwenyekiti wa ujumbe hiyo alisema.

"Sasa tunachunguza ripoti za kutisha za mashambulizi ya mara kwa mara dhidi ya raia na miundombinu ya kiraia, ikiwa ni pamoja na hospitali na shule."

Wataalam wa usalama wa chakula wameonya juu ya hatari kubwa ya njaa, hasa katika maeneo ya eneo la Darfur.

Mavuno ya nafaka yamepungua kwa karibu nusu ikilinganishwa na mwaka jana, na bei ya nafaka tayari imeongezeka maradufu au mara tatu katika maeneo yaliyoathiriwa na vita, kulingana na Shirika la Chakula Duniani (WFP).

"Kama wakazi wa mashambani hawawezi kubaki salama katika ardhi yao kupanda mimea yao au kuchunga mifugo yao, tutapata shida pia," alisema Joy Ezeilo mmoja wa wataalamu wa ujumbe huu.

"Nchini Sudan, maeneo ya ardhi ya kilimo yamegeuka kuwa viwanja vya vita, huku mashamba na biashara zikiwa zimetelekezwa huku watu wakikimbia kwa ajili ya usalama wao," shirika la WFP limesema katika taarifa.

"Kuna ukosefu mkubwa wa hela kote nchini, na kupunguzwa mara kwa mara kwa njia za mawasiliano huzuia juhudi za kuendeleza biashara. Bei za vyakula nchini Sudan ziko juu kwa asilimia 73 kuliko mwaka jana na asilimia 350 juu ya wastani wa miaka mitano, ikichochewa na kushuka kwa thamani ya sarafu hiyo," WFP imeongeza kusema katika taarifa yao.

WFP inasema madhara hayo yanaonekana nchini Sudan Kusini na Chad ambako biashara iliyotatizika na uhamishaji mkubwa wa watu unapunguza rasilimali na kuzidisha njaa.

TRT Afrika