'Hali ya kibinadamu Sudan imefikia pabaya' Umoja wa Mataifa

'Hali ya kibinadamu Sudan imefikia pabaya' Umoja wa Mataifa

Shehena za vifaa vya dharura zimetia nanga katika bandari ya Sudan
Watu wanaendelea kuwasili katika bandari ya  Sudan wakihepa vita nchini humo  / Photo: Reuters

Umoja wa Mataifa unasema vifaa muhimu kwa ajili ya kuokoa maisha ya watu vinazidi kuwa haba katika maeneo ya mijini yaliyoathirika zaidi, hasa Khartoum.

Familia zinatatizika kupata maji, chakula, mafuta na bidhaa nyingine muhimu.

"Gharama ya usafiri kutoka katika maeneo yaliyoathirika zaidi imepanda kwa kasi, na kuwaacha walio hatarini zaidi kushindwa kufika katika maeneo salama," amesema Martin Griffiths, Msaidizi wa Katibu Mkuu wa Masuala ya Kibinadamu na Mratibu wa Misaada ya Dharura, UNOCHA.

Griffiths anaongezea kuwa Upatikanaji wa huduma za afya za haraka, ikiwa ni pamoja na wale waliojeruhiwa katika vurugu, ni moja ya vikwazo vikali, na hii inaongeza hatari ya vifo vinavyoweza kuzuilika.

"Kuna uporaji mkubwa wa ofisi na ghala za mashirika ya kibinadamu unyangani huu umemaliza vifaa vyetu vingi. Tunatafuta njia za haraka za kuleta na kusambaza vifaa vya ziada," taarifa yake inasema.

Shirika hilo la UN linasema shehena yenye makontena matano ya vifaa vingine vya afya imefika kwenye bandari ya Sudan, ikisubiri idhini ya mamlaka.

Kamati ya Kimataifa ya Msalaba Mwekundu , ICRC pia imethibitisha kwamba vifaa vya matibabu kutoka Amman, Jordan hadi Port Sudan vimewasili Port Sudan.

"Tani nane za mizigo ya kibinadamu ni pamoja na vifaa vya upasuaji kusaidia hospitali za Sudan na watu wa kujitolea kutoka Chama cha Hilali Nyekundu cha Sudan (SRCS) ambao wanatoa huduma za matibabu kwa watu waliojeruhiwa katika mapigano," ICRC imesema katika taarifa.

ICRC inasema inatuma ndege ya pili iliyobeba vifaa vya ziada vya matibabu vya ICRC na wafanyikazi wa dharura.

TRT Afrika