Kiongozi wa zamani wa kijeshi wa Guinea Moussa "Dadis" Camara alikimbilia uhamishoni baada ya kunusurika jaribio la mauaji miezi kadhaa baada ya mauaji ya 2009. / Picha: AA

Mahakama ya Guinea siku ya Jumatano ilimhukumu kiongozi wa zamani wa kijeshi Moussa "Dadis" Camara kifungo cha miaka 20 jela baada ya kumpata na hatia ya uhalifu dhidi ya ubinadamu katika mauaji ya uwanja wa michezo ya mwaka 2009 yaliyofanywa na jeshi na kuua takriban watu 157 na kuwaacha makumi ya wanawake kubakwa.

Mahakama ya Jinai ya Guinea ilimtia hatiani Camara na maafisa wengine saba wa vyeo vya juu baada ya kesi ya muda mrefu juu ya mashtaka ya mauaji, utekaji nyara na ubakaji ambayo yalitajwa tena kama "uhalifu dhidi ya ubinadamu" siku ya Jumatano.

Washtakiwa wengine wanne waliachiliwa huru.

Zaidi ya manusura 100 na jamaa za wahasiriwa walitoa ushahidi katika kesi hiyo iliyoanza Novemba 2022, zaidi ya muongo mmoja baada ya mauaji hayo na huku kukiwa na shinikizo kutoka kwa familia na wanaharakati wanaodai haki itendeke.

Watu 'wasiyodhibitiwa'

Waandamanaji kwenye uwanja wa michezo Septemba 2009 walikuwa wakipinga mipango ya Camara kugombea urais wakati wanajeshi walipowafyatulia risasi na kuwabaka makumi ya wanawake. Kiongozi wa wakati huo wa kijeshi alikuwa amefanya mapinduzi mwaka uliopita.

Wanajeshi wakati huo walisema "watu wasiodhibitiwa" wa jeshi walifanya ubakaji na mauaji.

Lakini wasaidizi wakuu wa Camara walikuwa uwanjani na hawakufanya lolote kukomesha mauaji hayo, ripoti ya Human Rights Watch ilisema.

Wengi wa waliouawa kwenye maandamano ya uwanja huo walipigwa risasi, kuvunjwa au kupigwa visu hadi kufa huku baadhi ya wanawake wakitolewa nje kutoka mafichoni na kubakwa na genge la watu na wanaume waliovalia nguo za kijeshi kwa siku kadhaa, walioshuhudia walisema.

Wengi hawakuweza kukwepa risasi baada ya walinzi wa rais wa Camara kuzingira uwanja huo na kuziba njia za kutoka, walionusurika walisema.

Alikuwa amelala

Ilichukua siku kadhaa kabla ya familia za wahasiriwa kuruhusiwa kuja kuchukua miili, walisema wakati wa kesi hio ikisikilizwa.

Hata hivyo, wengi hawakupata miili ya jamaa zao.

Camara alikimbilia uhamishoni baada ya kunusurika jaribio la mauaji miezi kadhaa baada ya mauaji hayo lakini alirejea Guinea zaidi ya muongo mmoja baadaye.

“Madamu niko hapa mbele yako ni kwa sababu ya uzalendo wangu, la sivyo nisingekubali kuja,” alisema katika siku yake ya kwanza mahakamani ya kusomewa mashitaka mwaka 2022 na kuongeza kuwa alikuwa amelala wakati mauaji hayo yakitokea.

Akiwa jela mwishoni mwa mwaka jana, Camara aliachiliwa huru na watu wenye silaha ambao walivamia gereza kuu la nchi hiyo lakini alirudishwa rumande saa chache baadaye huku wakili wake akisema alikuwa ametekwa nyara.

TRT Afrika