Na Dayo Yusuf
Disemba 20, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo inaingia katika uchaguzi mkuu wenye umuhimu mkubwa.
Zaidi ya wapiga kura milioni 44 wamesajiliwa kushiriki shughuli hiyo. Pia watachagua kati ya makumi ya maelfu ya wagombeaji wa mabaraza ya ubunge na mitaa katika nchi yenye rasilimali nyingi zaidi Afrika, lakini imegubikwa na mizozo na ufisadi na ukosefu wa usalama.
‘’Nikona huzuni ndani ya moyo hata sina wakati wa kufikiria uchaguzi,’’ Kanyere Mbenda anaambia TRT Afrika.
Kanyere na wanawe watano wameishi katika kambi ya Don Bosco mjini Goma kwa zaidi ya miaka mitatu. Yeye pamoja na mamia wengine walikimbia mapigano yaliyozuka kati ya wanajeshi wa serikali na wapiganaji wa M23 katika wilaya ya Rutshuru mkoa wa Kivu ya Kaskazini.
Japo anafuatilia habari za uchaguzi, anahofia kuwa hakuna anayemjali yeye aliye kambini.
‘’Usiku na mchana ninalia, ninawaza namna tutakula mimi na watoto wangu hata kopo la mchele linalouzwa kwa bei nafuu hatupati kisha niende kumpigia kura nani?’’ anauliza.
Kanyere ni miongoni mwa raia milioni 6.9 wa DRC waliokimbia mapigano kutoka makazi yao katika mikoa ya Kivu na Goma, Mashariki mwa nchi.
Kwa mujibu wa shirika la Umoja wa Mataifa la wakimbizi UNHCR, mapigano mapya yaliyozuka tangu mwezi Oktoba katika eneo la Mashariki kati ya wapiganaji wa M23 na jeshi la taifa yamesababisha idadi kubwa zaidi ya wakimbizi wa ndani.
Nalo shirika la uhamiaji la kimtaifa ILO limetahadharisha kuwa mbali na wakimbizi wa ndani kunao wakimbizi wengine zaidi ya milioni moja waliohamia nchi za nje ya DRC kukimbia mapigano.
Watetezi wa haki za binadamu wamelalamikia kushindwa kwa serikali zilizotangulia na ile iliyoko madarakani kuleta amani katika eneo la Mashariki mwa nchi, eneo linaloaminiwa kuwa na utajiri mkubwa zaidi wa raslimali za madini na mali asili.
Huenda hii imevutia mamia ya makundi ya wapiganaji wanaodai kutetea maslahi ya wakaazi wa hapo dhidi ya unyonyaji unaofanywa na mashirika ya kigeni na vyombo vya serikali kupitia kandarasi zisizowajali.
Lakini huku makundi hayo yakiendelea kuzozana na majeshi ya serikali, wananchi wameendelea kupoteza maisha yao na nyumba zao zaidi huku uwekezaji katika maeneo hayo ukiwa wa chini zaidi.
Na sasa wananchi hao hao wanaotafuta watu wa kupwapigania na kuwahakikishia usalama wao, wanashindwa kushiriki upigaji kura kutokana na jambo hilo hilo , Usalama.
Kanyere na wakimbizi wengine walioko kambini wanasema kuwa almuradi hawajaangaliwa maslahi yao hawaoni haja ya kupiga kura.
''Mimi watakapoanza kunipatia chakula na watoto wangu, tutaelewana nao, na wanipe pia sehemu ya kuwalea watoto wangu,'' anasema Kanyere.
Wengine kama Salomon Munyandekwa alikimbia ghasia za waasi na familia yake na anaishi katika kambi, wilayani Rutshuru, amepoteza pia matumaini ya kushiriki uchaguzi huo .
''Tuko katika mateso sana. Sasa mtu mwenyewe anaishi kwa kuhangaika, na badala atoke kwenda kutafuta riziki unatarajia aje ashinde katika mstari wa kupiga kura mchana kutwa?'' anauliza Salomon.
Malalamiko yake ni kuwa hata wale waliosalia maeneo yao, wanaogopa kushambuliwa wakiwa katika shughuli ya kupiga kura.
''Unaona hiyo ni shida kubwa kwetu ambayo itasababisha wengi kati yetu wasishiriki kupiga kura,'' anaongezea Salomon.
Hata hivyo ni muhimu kutaja kuwa sio wakimbizi wote walio kambini wametoroka vita. Wengine wameathiriwa na mafuriko yaliyosomba makazi yao, au wamehama kukimbia maradhi.
Sababu hizi hizi zilisababisha mamilioni wengine kukosa upigaji kura katika uchaguzi uliotangulia.
Wakimbizi wa ndani wamesisitiza kuwa wangependa kupiga kura zao pia lakini wanataka kwanza serikali iwahakikishie usalama wao.
''Serikali ya Congo isikubali mazungumzo na maadui ili turudi kwa nyumba zetu na hapo ndipo tutashiriki uchaguzi tukiwa na furaha. Tungependa kufanya uchaguzi tukiwa na furaha kwasababu adui hatokuwepo,'' anasisitiza Salomon.
Kwa mujibu wa sheria za CENI, Tume inayosimamia uchaguzi nchini Jamhuri ya Demokrasia ya Congo, watu waliokimbia makazi yao hawawezi kushiriki uchaguzi.
Kumaanisha kuwa takriban Wakongomani milioni 8 walio kambini ndani na nje ya nchi hawatashiriki uchaguzi huu.
Katika uchaguzi uliopita wa 2018, wakongomani wengi walishindwa kushiriki uchaguzi kutokana na kukimbia makazi yao.
Mfano, Wakaazi wa eneo la Beni na Lubero Mashariki mwa nchi walikosa kupiga kura baada ya kukimbia makazi yao kutokana na ugonjwa wa Ebola uliotokea eneo hilo.
Wilaya ya Kwamouth wengi waliokimbia makazi yao ilikuwa kutokana na ukosefu wa Usalama.
Kwa mujibu wa Tume ya Uchaguzi CENI, wilaya za Rutsuru na Masisi hazitaweza kushiriki uchaguzi kutokana na ongezeko la uasi na mashambulio unaotishia usalama wa watu na kusababisha wengi hata hivyo kukimbia makazi yao.
Katika muda wa miezi miwili iliyopita, kumekuwa na madai ya waasi wa M23 kuwa wameteka baadhi ya vijiji Mashariki na Kusini Mashariki mwa nchi na hivyo kuongeza wasiwasi zaidi ya watu kutoshiriki uchaguzi baada ya kukimbilia usalama.