Serikali ya Ghana imeahidi fedha zaidi kwa ajili ya mpango wa kuwalisha wafungwa baada ya mamlaka ya magereza kufichua kuwa walikuwa wakikabiliwa na changamoto za kuwalisha wafungwa.
Serikali imekuwa ikitumia wastani wa Cedi 1.80 za Ghana ($0.16) kulisha kila mfungwa kila siku, Isaac Kofi Egyir, mkurugenzi mkuu wa jeshi la magereza la Ghana, aliiambia kamati ya hesabu za bunge katika mji mkuu wa Accra siku ya Ijumaa.
Kufikia Mei 2022, magereza katika nchi hiyo ya Afrika Magharibi yalikuwa na takriban wafungwa 14,097 licha ya kuwa na uwezo wa kumudu wafungwa 9,945, Jeshi la Magereza la Ghana lilisema wakati huo.
Siku ya Ijumaa, wajumbe wa bunge walielezea kushangazwa na nmana wakuu wa magereza walikuwa wakimudu kulisha mtu mmoja $0.16 pekee, kila siku.
Msongamano wa wafungwa
Egyir alisema huduma ya magereza inamiliki mashamba ya mazao ya chakula, ambayo yanasaidia katika kuongeza chakula kinachopatikana kwa kutumia fedha za serikali.
“Tunayo mashamba kote nchini. Ni mashamba yetu ambayo yametuwezesha tangu matatizo ya kulisha kutokea. Hilo ndilo tunalofanya ili kukamilisha juhudi za serikali katika kuwalisha wafungwa,” Egyir alisema.
Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani Naana Eyiah alisema serikali itaongeza kiwango cha wastani cha pesa kilichotengwa kwa ajili ya chakula cha kila siku cha kila mfungwa, shirika la habari la Ghana linaripoti.
Egyir alisema msongamano pia bado ni changamoto kuu katika magereza ya Ghana.
Kiwango cha msongamano, hata hivyo, kilipungua kutoka 72.41% mnamo 2007 hadi 41.7% kufikia Mei 2022.
TRT Afrika na mashirika