Thomas Sankara alichaguliwa kuwa Rais wa Burkina Faso akiwa na umri wa miaka 33, aliuwawa akiwa madarakani miaka minne baadae. Picha : AP

Na Mubarak Aliyu

TRT Afrika, Afrika Magharibi

Safari ya kumpata Sankara mpya imechochea vurugu na machafuko mengi ya kisiasa nchini Burkina Faso toka mwaka 2014, wakati utawala wa muda mrefu wa Blaise Compaoré ulipoondolewa kupitia maandamano ya wananchi.

Hata hivyo, Sankara wa kipindi hicho asingeweza kuhimili muktadha wa kipindi cha kisiasa cha wakati huu, kwani kumetokea mabadiliko mengi toka miaka ya 1980.

Thomas Sankara atakumbukwa tu si kama kiongozi wa Burkina Faso, bali mtu aliyekuwa mstari wa mbele katika kutekeleza sera za kijamii na kiuchumi, zilizolenga kumuinua mwananchi wa kawaida katika nchi hiyo inayopatikana Magharibi mwa Afrika.

Juhudi zake kubwa na mafanikio yake katika kukuza elimu na kuboresha huduma za afya na usawa kijinsia, zilitengeneza mazingira wezeshi ya kuwa na mandeleo asilia Barani Afrika.

Hata hivyo, ni vyema kuangazia namna Sankara alivyoingia madarakani, kwani bado kinabaki kuwa kama kikwazo cha kumpata mtu mwenye haiba kama yake.

Kupanda kwa Sankara

Mapinduzi ya 1983, yaliyosukwa na swahiba wake mkubwa Blaise Compaoré na wenzake wengine jeshini yalifanikiwa kuuondoa utawala wa Ouédraogo madarakani, na kuanzishwa kwa Baraza la Mapinduzi Kitaifa, liliongozwa na Sankara mwenyewe.

Mabadiliko ya kisiasa yaliyofuatia chini ya Sankara yalijumuisha kuondolewa kwa vongozi wa jadi nchini humo pamoja na maamuzi ya kupunguza matumizi yasiyo ya lazima serikalini, ambayo Sankara mwenyewe aliyaona ni kama upetevu bure wa pesa.

Hata hivyo, kadiri muda ulivyozidi kwenda, ndivyo viongozi wengine wa juu, akiwemo Compaoré, walivyoonesha wazi kutofurahishwa kwao na maamuzi ya Sankara.

Hisia hizi zilipelekea mpasuko mkubwa ndani ya jeshi, moja likimuunga mkono Sankara na lingine likiwa upande wa Compaoré.

Na ilipofika mwaka 1987, Sankara aliuawa katika mapinduzi yaliyohusisha umwagaji damu, yaliyongozwa na Compaoré, kupitia msaada mkubwa wa kijeshi kutoka nje ya Burkina Faso.

Mataifa mengi ya magharibi yalionesha hofu ya sera za Sankara, wakiamini kwamba zitafifisha ushawishi wao barani Afrika./Picha:AFP

Wafuasi wa Sankara dhidi ya wa Compaoré

Hata leo, hali ya kisiasa nchini Burkina Faso imegawanyika, kati ya wanaomfuata Sankara na wale wenye kumuunga mkono Compaoré, kundi la kwanza likikumbatia maendeleo zaidi wakati la pili linaonekana kuwa la kihafidhina tu.

Ni dhahiri shahiri kwamba, hali ya sasa kisiasa nchini Burkina Faso, bado ina akisi mzozo wa madaraka nchini humo, toka kuuwawa kwa Sankara mwaka 1987.

Mnamo 2003, wanajeshi wasiopungua 16 walikamatwa huko Ouagadougou, kwa madai ya kupanga njama za kufanya mapinduzi.

Kati ya waliokamatwa ni Michel Norbert Tiendrebéogo, kiongozi wa chama chenye mrengo wa Sankara, kilichojulikana kama Socialist Military Front.

Jaribio hilo la mapinduzi ndilo lililoweka mazingira ya kukosekana kwa utulivu wa kisiasa, hasa kati ya wafuasi wa Sankara na wa Compaoré.

Anguko la Compaoré

Hatimaye, baada ya miaka 27, kiongozi huyo alifurushwa madarakani kupitia maandamano ya waburkinabe ya mwaka 2014.

Miaka saba baadae, ulianzishwa uchunguzi wa uhusika wake katika mauaji ya Sankara, jambo lililopelekea kuhukumiwa kwake, yeye pamoja na washirika wake wawili.

Hata hivyo, serikali ya kiraia ilipinduliwa na jeshi mnamo mwaka 2022 na mara moja Burkina Faso ikawa chini ya utawala wa kijeshi, unaoongozwa na Paul-Henri Sandaogo Damiba.

Ingawa mapinduzi hayakuwa sababu ya hukumu ya Compaoré, bado kulikuwa na wafuasi wa kiongozi huyo wa zamani kuhusika, japokuwa Damiba alihusisha fikra za Sankara kama sababu iliyompa motisha kutwaa madaraka kijeshi.

Blaise Compaoré alikana kuhusika katika mauaji ya Sankara. Hata hivyo naye aliondolewa madarakani. Picha: /AFP

Miezi kadhaa baada ya mapinduzi, serikali ya Damiba ilimualika Compaoré kuhudhuria mkutano wa maridhiano wa marais wa zamani katika mji mkuu wa Ouagadougou, na kumruhusu rais wa zamani aliyehukumiwa na aliyejitenga kurejea Burkina Faso kwa siku kadhaa na hatimaye kuondoka bila kukamatwa.

Ujio wa Ibrahim Traore

Dharau na kutokuadhibiwa kwa Compaoré baada ya kutoka uhamishoni Ivory Coast, kulimuibua Ibrahim Traore mwaka 2022, kufuatia mapinduzi mengine ya kijeshi dhidi ya utawala wa Damiba.

Mapinduzi ya Traoré bado yanadhihirisha madhara yanayotokana na jitihada za kumrithi Sankara katika siasa za Burkina Faso.

Kwa kuzingatia sera za kupinga ubeberu za Ibrahim Traoré, haikushangaza wakati jeshi lilipotangaza jaribio la mapinduzi lililoshindikana mnamo Septemba 2023, na kuonyesha uwezekano wa kunyakua madaraka zaidi.

Hali hii ya ukosefu wa utulivu kisiasa, inaturudisha nyuma mpaka kwenye mauaji ya Sankara, yaliyosukwa na mataifa ya kigeni, huku yakimhusisha Compaoré kwa kiasi kikubwa.

Kapteni Ibrahim Traore alimpindua Roch Kaboré, miezi nane baada ya kuondolewa madarakani kwa  Paul-Henri Sandaogo Damiba . /Picha : Wengine

Sankara mjamaa wa kweli

Kama ilivyo ada ya kipindi hicho, urithi wa Sankara ulihusanishwa na siasa za vita baridi, wakati ambapo maslahi ya kijiografia yalikuwa na ushawishi mkubwa kupata nafasi za kisiasa barani Afrika.

Kama mjamaa, Sankara alitishia maslahi ya mataifa makubwa ya magharibi.

Katika miaka ya hivi karibuni, mapambano ya madaraka yameanza upya, sura mpya zikitamalaki.

Kutawala kwa bendera za kirusi, hasa wakati wa maandamano yenye kuunga mkono jeshi, yanakuja na hofu mpya, hali inayoenda kinyume na urithi na fikra za Sankara mwenyewe.

Katika msingi wake, harakati za kupinga ubeberu ni lazima ieleweke kama mapambano ya uhuru, badala ya kutegemea upande mmoja wa mgawanyiko wa mamlaka ya kimataifa.

Hivyo, ni jukumu la viongozi wa Burkina Faso kupanga njia mpya ya utawala itakayoongozwa na watu, ikoongozwa na historia yenye kukidhi sifa za jamii zake.

Sankara ajaye?

Thomas Sankara aliuwawa akiwa na miaka 37, Oktoba 15, 1987 mjini  Ouagadougou./  Picha: AP

Pia ni wajibu wa watu wa Burkinafaso na Waafrika kwa ujumla, kuyafanyia kazi mawazo chanya kutoka kwa urithi wa Sankara ili kukuza mbinu mpya za utawala bora, kinyume na kuunga mkono mapinduzi ya kijeshi kwa matumaini ya kupatikana kwa Sankara mpya.

Ni vyema kutilia maanani kwamba, fikra za Sankara hazikufungamana na upande wowote.

Mubarak Aliyu ni mchambuzi wa masuala ya Kisiasa na ya Kiusalama kwa ukanda wa Sahel na Afrika Magharibi.

TRT Afrika