Ethiopia yasema Tanzania kuongoza maongezi ya amani kati yake na kundi la kigaidi, OLA

Ethiopia yasema Tanzania kuongoza maongezi ya amani kati yake na kundi la kigaidi, OLA

Mnamo Mei 2021 serikali ya Ethiopia ilitangaza kuwa kikundi cha kijeshi cha Oromo Liberation Army ni kundi la kigaidi
Waziri mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed anasema hakuna faida itakayotokana na vita  / Photo: AP Archive

Ethiopia imesema itaanzisha mazungumzo ya amani na kundi ambalo serikali ililitangaza kama kundi la kigaidi, Jeshi la Ukombozi la Oromo yaani Oromo Liberation Army, OLA. OLA iko katika eneo la Oromia eneo kubwa zaidi nchini Ethiopia linaloenea kutoka magharibi hadi mashariki mwa nchi.

"Mazungumzo na OLA yataanza Tanzania siku moja baada ya kesho," Waziri Mkuu Abiy Ahmed alisema Jumapili katika hafla iliyosherehekea maendeleo ya mchakato wa amani kati ya serikali na chama cha Tigray People Libertarian Front, TPLF, ambacho kimemaliza mzozo mkali nchini kaskazini mwa nchi.

OLA ilitambulika na bunge la Ethiopia kama kundi la kigaidi mnamo Mei 2021. Serikali imelaumu OLA kwa mauaji katika eneo la Oromia nchini humo.

"Serikali na watu wanataka sana mazungumzo haya, hakuna faida itakayotokana na vita," Ahmed alisema.

Jeshi la OLA limejibu kwa kukubali swala la maongezi ya amani.

"Utawala wa Ethiopia umekubali masharti yetu ya mazungumzo ya amani, ambayo ni pamoja na kuhusika kwa mpatanishi huru wa na kujitolea kudumisha uwazi katika mchakato mzima," OLA imesema katika taarifa yake kwa vyombo vya habari.

"OLA bado haijayumba katika kujitolea kwake kushiriki katika mazungumzo yenye kujenga azimio la amani ambalo linashughulikia malalamiko na matarajio ya watu wa Oromo."

Tanzania bado haijatoa maelezo yoyote kuhusu mchakato wa amani ambao Ethiopia inasema itakuwa mwenyeji.

Kundi la jeshi la Oromo Liberation Army, OLA ni akina nani ?

Mwaka wa 1974 kundi lililojitenga la Oromo Liberation Front, OLA, ambalo lilikuwa kundi la kisiasa lililoanzishwa kwa lengo la kutetea haki za binadamu, na usawa wa watu wa Oromo.

Katika miaka ya 1980, OLF ilipigana pamoja na makabila mengine nchini Ethiopia dhidi ya utawala tawala wa Derg, ambao ulitawala nchi hiyo kwa miaka 17.

Wakati utawala wa Derg ulipopinduliwa miaka ya 1990, uongozi wa Ethiopia ulichukuliwa na chama cha Ethiopian People's Revolutionary Democratic Front, EPRDF, muungano wa vyama vya kikabila.

Serikali ya Ethiopia imelaumu kikundi cha OLA kwa mauaji katika eneo la Oromia   

EPRDF ilitofautiana na Kundi la Ukombozi wa Oromo (OLF) baada ya OLF kukataa kuacha lengo lao la kujitenga kwa eneo la Oromia kutoka Ethiopia. Wananchama wa OLF walialazimika kukimbilia Eritrea na kuanza mapambano ya silaha dhidi ya EPRDF.

Mnamo 2011, OLF ilitangazwa kama shirika la kigaidi na serikali ya Ethiopia. Mnamo 2018, Ethiopia ilipata serikali mpya chini ya waziri mkuu Abiy Ahmed.

Bunge liliondoa Muungano OLF kutoka kwenye orodha ya mashirika ya kigaidi na wanachama wa OLF walipewa msamaha na kuruhusiwa kurejea Ethiopia.

Mmoja wa makamanda wa OLF, Kumsa Diriba alishindwa kufikia makubaliano na serikali juu ya kuwapokonya silaha wapiganaji wa OLF.

Mnamo 2019, OLA ilijitenga rasmi na kikundi cha Oromo Liberation Front. Kundi lililogawanyika la Diriba liliendelea kupigana dhidi ya serikali ya Abiy Ahmed.

Serikali imekuwa ikilaumu OLA kwa mauaji katika eneo la Oromia nchini humo ambayo yalisemekana kuwa ya kikabila. OLA ilifanya makualiano na chama cha Tigray People’s Liberation Front, TPLF, mwaka 2021. TPLF ililipigana dhidi ya serikali kwa miaka miaka miwili tangu Novemba 2020 kaskazini mwa nchi.

Mnamo Mei 2021 serikali ya Ethiopia ilitangaza OLA (OLF-Shene) kama kundi la kigaidi.

Na sasa serikali ya waziri mkuu Abiy Ahmed imeweka wazi nia ya kuwa na mazungumzo ya amani na kundi hilo.

TRT Afrika