Emmanuel Nchimbi achaguliwa kuwa Katibu Mkuu mpya CCM. Picha/Wizara Mambo ya Nje Tanzania. 

Wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa wa chama tawala nchini Tanzania CCM, iliyoketi mjini Unguja imemtua balozi Emmanuel Nchimbi kuwa Katibu Mkuu wa Chama hicho. Nchimbi anarithi nafasi hiyo kutoka kwa Daniel Chongolo, ambaye alijiuzulu Novemba, 2023.

Rais Samia Suluhu Hassan ambae ndie mwenyekiti wa CCM akisalimiana na Katibu Mkuu mpya wa CCM Emmanuel Nchimbi. Picha/CCM.

Chongolo alifikia hatua ya kujiuzulu nafasi hiyo nyeti ndani ya chama hicho tawala nchini Tanzania, kufuatia madai ya kuchafuliwa kwenye mitandao ya kijamii.

Nchimbi anakuwa mwanasiasa wa pili kuchaguliwa kushika nafasi hiyo nyeti ndani ya chama tawala, chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan ambaye pia ni Mwenyekiti wa chama hicho.

Akiwa ameanzia harakati zake za kisiasa kama Mwenyekiti ndani ya Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM), Nchimbi amewahi pia kuwa mbunge na pia kuhudumu kama Waziri wa Habari na pia Waziri anayeshughulikia Mambo ya Ndani kwa nyakati tofauti.

Anapoanza majukumu yake mapya ndani ya CCM, Nchimbi atakuwa na kazi nyingi kiutendaji, zikiwemo kusimamia utekelezaji wa mipango mbalimbali ya kichama na shughuli za kila siku za uendeshaji wake.

Kazi kubwa nyingine inayomsubiri Nchimbi ni kudhibiti makundi ndani ya chama hicho tawala, suala ambalo limekuwa likikigawa chama hicho hasa nyakati za uchaguzi mkuu.

Hali kadhalika, Nchimbi atakuwa na kazi ya kudhibiti nidhamu ndani ya chama, na kuhakikisha hakuna makundi yanayojitokeza baada ya uchaguzi na wakati wote ili kiendelee kuwa na umoja.

Uteuzi wake unakuja wakati chama hicho kikongwe nchini Tanzania, kinajiandaa na uchaguzi wa Serikali za Mitaa baadaye mwaka huu, na Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Mwakani.

TRT Afrika