Nchi wanachama ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) zimejidhatiti kukuza biashara ya ndani, ukusanyaji wa rasilimali na kukaribisha mataifa mapya kwenye umoja huo.
Mapema wiki hii, Katibu Mkuu wa Jumuiya hiyo, Peter Mathuki amesisitiza haja ya kuimarisha biashara ya ndani ya kanda kwa kuboresha utekelezaji wa itifaki za Umoja wa Forodha wa EAC na Soko la Pamoja.
Katika salamu zake kwa wananchi wa Afrika Mashariki, Mathuki aliweka msisitizo kwenye haja ya kufanya kazi kwa pamoja ili kuondoa Vikwazo Visivyo vya Ushuru (NTBs) vinavyozuia biashara ya ndani ya kanda, huku akionyesha matumaini ya kuongezeka kwa biashara ya ndani ya kikanda, hadi kufikia walau asilimia 40, ndani ya miaka mitano ijayo.
Kulingana na Katibu Mkuu huyo, ni dhamira ya dhati ya nchi wanachama wa EAC kutekeleza Ushuru wa Pamoja wa Nje (CET) na kufikia hadhi nne, ili kuongeza ushindani wa kibiashara na kukuza sekta ya viwanda.
”Ukanda wetu ulipitisha muundo wa CET kuanzia asilimia sifuri mpaka 35, vivyo hivyo tunajitahidi kuendelea na utekelezaji wake ili kuwezesha ushindani wa kibiashara na kukuza sekta ya viwanda katika ukanda huu,” aliongeza.
Akizungumzia hali ya Shirikisho la Kisiasa, Mathuki alitanabahisha kuwa, kufuatia agizo lililotokana na Mkutano wa 23 wa Wakuu wa Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki, Jumuiya hiyo itafanya kazi kwa ukaribu na serikali za Tanzania, Sudan Kusini, Rwanda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ili kuharakisha mashauriano ili kufikia hatua hiyo muhimu ya uwepo wa Jumuiya hiyo inayoundwa na nchi nane, ikiwa na makao makuu yake mjini Arusha, Tanzania.
"Wataalamu hao wanatarajiwa kuwasilisha ripoti kuhusu muundo pendekezwa wa Shirikisho la Kisiasa la EAC na kuandaa Katiba ya Shirikisho hilo kama mfano wa mpito wa Shirikisho la Kisiasa," alisema.
Idadi ya watu katika Jumuiya hiyo, ambayo ndio inayoongoza kwa utangamano kwa sasa barani Afrika, imefikia milioni 302, hasa baada ya kuongezeka kwa Somalia, ambayo ilijiunga na Jumuiya mwishoni mwa mwaka jana.