Na Edward Qorro
TRT Afrika, Istanbul, Uturuki
Septemba 11, itaendelea kubakia siku ya kipekee kwa watu wa Marekani na ulimwengu mzima.
Miaka 22 iliyopita, washambuliaji kadhaa wa kujitoa mhanga, waliteka ndege nne za abiria za Marekani na kuzigongesha kwenye majengo nyeti ya umma nchini humo.
Ndege mbili ziligonga Kituo cha Kimataifa cha Biashara (WTC) na nyingine ilianguka katika Wizara ya Ulinzi ‘Pentagon’ ambako zaidi ya watu 2,000 walifariki dunia na zaidi 5,000 walijeruhiwa.
Majengo hayo maarufu nchini Marekani yalishika moto, na ndani ya muda mfupi, majengo hayo yenye ghorofa 110 kila moja, yaligeuka kuwa majivu.
Takribani watu 2,996 walipoteza maisha katika tukio hilo, huku asilimia kubwa ya vifo hivyo vikiripotiwa katika jiji la New York.
Vita dhidi ya Ugaidi
Mashambulizi hayo yalimsukuma Rais wa Marekani wa wakati huo, George W. Bush kutangaza vita vikubwa dhidi ya ugaidi, huku Afghanistan na Iraq zikilengwa zaidi.
"Tukio hilo, japo limetokea katika ardhi ya Marekani, bado limeumiza mioyo ya ulimwengu mzima. Dunia nzima inakuja pamoja kwa ajili ya vita vipya, vya kipekee ndani ya karne ya 21. Hivi ni vita dhidi ya wale wanaochochea ugaidi na serikali zote zinazounga mkono dhuluma hii," alisema Rais Bush.
Ilipofika Septemba 24, Rais Bush alitangaza kuzuia mali zote za vikundi vya kigaidi. Na huu ndio ukawa mwanzowa jitihada za kupigana vita dhidi ya ugaidi ulimwenguni.
Uko upande wetu au dhidi yetu?
"Hivi ndivyo Marekani ilipoanza kusaka nadharia mbalimbali za kujihami, ikiwemo kuziwekea vikwazo baadhi ya nchi ambazo ziliendelea kuunga mkono ugaidi duniani," mhadhiri mwandamizi kutoka Chuo cha Diplomasia nchini Tanzania (CFR), Dkt Jason Nkyabonaki anaiambia TRT Afrika.
Kulingana na Dkt Nkyabonaki, hapa ndipo Marekani ilipoanza kuchagua washirika wake kwa nadharia maarufu ya kama 'uko upande wetu au upande wa adui zetu'.
Baadhi ya nchi ambazo ziliathirika na vikwazo kutoka Marekani wakati wa vita yake dhidi ya ugaidi ni pamoja na Cuba, Jamhuri ya Watu wa Korea (Korea Kaskazini), Iran na Syria.
"Huu ulikuwa ni ubatizo wa moto," anaeleza.
Kulingana na mhadhiri huyo, Marekani ilisitisha kufanya biashara na kuendeleza mahusiano ya kidiplomasia na nchi zilizounga ugaidi duniani.
Mabadiliko ya Kiusalama
Tofauti na ilivyokuwa kabla ya tukio la Septemba 11, kwa sasa itamlazimu abiria wa ndege kupita kwenye vituo kadhaa vya upekuzi kabla ya kupanda chombo hicho cha usafiri.
Sahau kuhusu ule upekuzi wa kawaida tu, kwa sasa ili upande ndege itakupasa uweke wazi kila ulichokibeba ndani ya mifuko au mabegi yako.
Kama si kwa macho ya binadamu, basi vile ulivyovibeba vitaonekana kupigia mashine za kisasa zaidi.
Iwe katika viwanja vya ndege, au hata vile vya michezo; hali ya ulinzi na usalama imebadilika kwa kiasi kikubwa sana.
"Hatua hii imelazimu baadhi ya nchi kuwekeza zaidi katika kudhibiti ugaidi kuliko kukabiliana na ugaidi wenyewe," anasema Dkt Nkyabonaki.
Siku hizi, limekuwa ni jambo la kawaida kabisa kuona wasafiri wakisimama kwenye mistari mirefu kwenye vituo vya ukaguzi vya usalama, kwa muda unaoweza kuzidi hata saa moja.
Wataalamu wa usalama wa usafiri wa anga wanakiri kwamba kabla ya tukio la Septemba 11, hakuna aliyewahi kuwaza kuwa itatokea siku moja magaidi watatumia ndege za abiria kufanya maangamizi na mauaji ya watu wasio na hatia.
"Maoni yangu ni kwamba mfumo wa utawala wa kimataifa ulibadilika kabisa huku mataifa yakiboresha mifumo yao ya kijeshi na usalama. Hata hivyo, changamoto za kigaidi badi ni tatizo kubwa sana, hasa katika mataifa dhaifu."