Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu (AfCHPR) imetenga Februari 12 na 13 kama siku za kusikiliza shauri la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) dhidi ya Rwanda, ambalo limefunguliwa kwenye mahakama hiyo iliyoko jijini Arusha, nchini Tanzania.
DRC ilifungua kesi dhidi ya Rwanda, Agosti 21 2023, ikiituhumu nchi hiyo kwa ukiukwaji mkubwa wa haki za kibinadamu.
Kupitia kesi namba 007/2023, DRC inaitihumu Rwanda kuhusika na mgogoro unaoendelea Mashariki mwa DRC.
DRC inadai kuwa mgogoro huo umesababisha mauaji makubwa ya watu, milipuko ya magonjwa kama vile kipindupindu, uharibifu wa shule na watu na vile vile kusababisha watu 520,000 kukosa makazi.
Pia imedai kuwa nchi hiyo inahifadhi watuhumiwa mbalimbali wa kihalifu ambao vibali vyao vya kukamatwa vimekwisha kutolewa.
DRC imeiomba mahakama hiyo yenye makao makuu yake jijini Arusha, Tanzania kuiwajibisha Rwanda na kuiamrisha kuondoka vikosi vyake nchini DRC na kuacha kutoa msaada kwa kikundi cha waasi wa M23.
Hata hivyo, Rwanda imepinga hatua ya mahakama ya AfCHPR kusikiliza shauri hilo, ikisema kuwa haina uhalali wa kusikiliza kesi hiyo.