DRC inasema mzozo huo uliwafurusha zaidi ya watu milioni 2.3 kutoka nyumba zao na kupelekea uharibifu wa mamia ya shule. / Picha: AFP

Kwa mara nyingine, Kinshasa imepiga kengele juu ya janga la kibinadamu lililosababishwa na "uchokozi" wa Rwanda ndani ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), siku chache kabla ya Mkutano mkuu wa Umoja wa Mataifa utakaoanza wiki ijayo.

Kwenye kikao na waandishi wa habari katika mji mkuu siku ya Alhamisi, Waziri wa mawasiliano Patrick Muyaya na Waziri mwenza wa Sheria Rose Mutombo wametoa malamiko hayo dhidi ya Kigali wakirudia madai ya kwamba Rwanda imekuwa ikiunga mkono waasi wa M23 walioongozwa na Watutsi, madai ambayo Kigali imekuwa ikikanusha mara kwa mara.

Kundi hilo la M23 kimechukua maeneo mengi Katika maeneo ya Kivu Kaskazini, maeneo ya mpaka wa nchi hizo mbili, tangu kuchukua silaha tena mwishoni mwa 2021 baada ya miaka kadhaa ya bila kufanya chochote.

Muyaya alitaja "uthibitisho usioweza kupingwa wa shughuli za uhalifu zinazoendeshwa na jeshi la Rwanda na wafuasi wake wa M23."

Aidha ameongeza kuwa mzozo huo umewalazimu zaidi ya watu milioni 2.3 kukimbia makwao na kuacha mamia ya shule zikiharibiwa au kuchukuliwa.

Pia imesababisha uharibifu "usiohesabika" katika Mbuga ya Kitaifa ya Virunga.

Msaada wa kidiplomasia

Mzozo huo pia umetajwa kusambaratisha mipango ya uchaguzi mkuu ujao wa Desemba kwani imefanya usajili wa wapigaji kura haswa katika maeneo yaliyoathiriwa na vita hivyo kutowezekana.

Wataalam wa UN wameishutumu Rwanda kwa kuunga mkono hundi hilo la waasi, na mnamo mwezi Julai, EU ililaani uwepo wa wanjeshi wa nchi hiyo mashariki mwa DRC.

Mnamo Agosti, Washington ilitangaza kuwakea vikwazo watu sita, raia wa Rwanda na DRC wakiwemo viongozi wa waasi, na kusema kuwa wamechangia kuongezeka kwa mgogoro wa hivi karibuni mashariki mwa DRC.

Waziri Muyaya, amekaribisha uungwaji mkono wa kidiplomasia wa hivi karibuni, na kutoa wito wa majibu ya nguvu zaidi ya kimataifa kwa mgogoro huo.

AFP