Katika uteuzi wa kwanza tangu kuchukua nafasi ya rais mnamo Januari 2019 Rais wa DRC, Felix Tshisekedi alifanya mabadiliko makubwa katika uongozi wa jeshi la polisi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo siku ya Jumapili, zaidi ya miaka minne baada ya kuingia madarakani.
TRT Afrika imeongea na bwana Philemon Ndambi wa Ndambi akiwa ni mchambuzi wa masuala ya siasa, na amesema kuwa uteuzi huo wa polisi miezi chache kabla ya uchaguzi ni kumpa nguvu Rais Tshisekedi na anahofia kuwa viongozi hao walioteuliwa, ni watu wake wa karibu.
"Isije ikawa wamewekwa kwa ajili yakutekeleza maamuzi ya kiongozi badala yakufanya kazi yao ya kulinda wananchi maana polisi, hapo nyuma, wameshawahi kushtumiwa kwa ukiukwaji wa Haki za Binadamu." Amesema Ndambi wa Ndambi.
Kupitia mfululizo wa maagizo yaliyosomwa kupitia televisheni ya umma, Benjamin Alonga Boni, Makamu wa Gavana wa sasa wa jimbo la Ituri, aliteuliwa kuwa Kamishna Mkuu wa polisi.
Kamishna wa Tarafa Raüs Chalwe Muntutu Ngwashi ameteuliwa kuwa Makamu wa Gavana wa Jimbo la Ituri na kuacha wadhifa wa Mkurugenzi wa Ukaguzi Mkuu wa Polisi wa Kitaifa.
Sylvano Kasongo ameacha nafasi ya kamanda wa polisi katika mji mkuu Kinshasa akielekea ofisi ya Commissariat General, ambapo ameteuliwa kuwa naibu kamishna mkuu wa polisi anayesimamia operesheni na ujasusi.
Rais Tshisekedi amemteua Naibu Kamishna wa Tarafa Jean-Bosco Galenga Makongo kuwa Mkuu wa polisi Mjini Kinshasa.
Juvenal Ibideko ameteuliwa kuwa Inspekta Jenerali wa Polisi.