Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC alisema atarahisisha hatua ya utawala wa kijeshi katika eneo la mashariki lililokumbwa na mzozo na kuondoa baadhi ya vikwazo vya usalama vilivyowekwa zaidi ya miaka miwili iliyopita.
Serikali iliamua maeneo hayo yazungukwe na vikosi vya usalama mwaka 2021, na hapo kuruhusu wanajeshi na polisi kuchukua udhibiti kutoka kwa taasisi za kiraia, kwa ajili ya kujaribu kukomesha ghasia zinazoongezeka katika maeneo hayo.
Rais Felix Tshisekedi siku ya Alhamisi, aliliambia taifa lake katika hotuba kwamba kutakuwa na taratibu katika majimbo ya Kivu Kaskazini na Ituri, ambayo itahusisha kukomesha marufuku ya kutotoka nje, kuruhusu maandamano ya amani na watu kuishi maisha ya kawaida.
Tangazo hilo linakuja zaidi ya miezi miwili kabla ya uchaguzi wa rais, wakati Tshisekedi anatarajia kuwania muhula wa pili katika uchaguzi wa 20 Desemba mwaka huu.
Changamoto ya usalama Kivu Kaskazini
Zaidi ya makundi 120 yenye silaha yanapigana katika eneo hilo, hasa kwa ajili ya ardhi na udhibiti wa migodi yenye madini ya thamani.
"Nimechukua azimio thabiti lkwa wakazi wa majimbo ya Ituri na Kivu Kaskazini ya kurahisisha utawala wa taratibu, hatua kwa hatua na kuzuia hali ya kuzingirwa," alisema Tshisekedi.
Mashirika ya kiraia na makundi ya kutetea haki za binadamu yamekosoa hali ya kuzingirwa, yakishutumu vikosi vya usalama kwa kutumia mamlaka yao dhidi ya wakazi.
"Serikali imeshindwa katika madhumuni yake yaliyotajwa ya kuboresha kwa haraka hali ya usalama. Mamlaka za kijeshi badala yake zimetumia uwezo wao usio wa kawaida kudhoofisha zaidi haki za watu bila kuadhibiwa, ikiwa ni pamoja na uhuru wa kujieleza na kukusanyika, na haki ya haki," ilisema Amnesty International.
Licha ya utawala wa kijeshi, ghasia katika eneo hilo zimeendelea kuongezeka. Inadaiwa wanamgambo wamepanua uwepo wao katika eneo hilo huku makundi ya waasi kama M23 wakiteka miji, na kuwafanya makumi ya maelfu ya watu kuyahama makaazi yao.