Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC imefikia kiwango cha kutokuwa na vifo vinavyotokana na maambukizi ya ugonjwa wa Mpox, imesema Wizara ya Afya ya nchi hiyo.
Wizara hiyo imesema kuwa kiwango cha vifo vinavyohusiana na janga la Mpox kilipungua kutoka 0.41% hadi 0% katika kipindi cha wiki moja.
Wizara pia imetangaza kuzinduliwa kwa awamu ya pili ya kampeni ya chanjo ya Mpox huku Equateur, Sud-Kivu, Tshopo, Sankuru na Bas-Uele yakiwa miongoni mwa majimbo yaliyoathiriwa zaidi na janga hilo.
Tangu kuanza kwa janga hili, DR Congo imerekodi maambukizi 53,860 yanayoshukiwa kuwa ya Mpox na vifo 1,255.
Kiwango cha jumla cha vifo kwa kesi zinazoshukiwa ni 2.33%, chini kidogo kutoka 2.39% wiki iliyopita.
Vituo vya Afrika vya Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa, yaani Africa CDC mnamo Agosti 14 vilitangaza janga la Mpox kuwa dharura ya afya ya umma.