Kiongozi wa chama cha upinzani cha ACT -Wazalendo cha nchini Tanzania Dorothy Semu./Picha: Wengine

Kiongozi wa chama cha upinzani cha ACT -Wazalendo cha nchini Tanzania Dorothy Semu ameweka wazi nia yake kugombea nafasi ya Urais wa nchi hiyo ifikapo mwezi Oktoba 2025.

Mwanasiasa huyo amesema kuwa yuko tayari kukabiliana na Rais Samia Suluhu Hassan katika Uchaguzi Mkuu wa 2025, iwapo chama chake kitampa ridhaa ya kufanya hivyo.

Kulingana na kiongozi huyo wa ACT-Wazalendo, kuna mapungufu makubwa nchini Tanzania yanayohitaji uongozi thabiti, uwazi na wenye malengo halisi kwa manufaa ya Watanzania wote, huku akibainisha masuala kadhaa ambayo atakabaliana nayo iwapo atapewa ridhaa ya kuiongoza nchi hiyo.

Semu amesema kuwa atahakikisha kuwa atapambana na kushika kwa kasi ya ukuaji uchumi, kupanda kwa gharama za maisha, changamoto ya ukosefu wa ajira kwa vijana pamoja na udhaifu katika usimamizi wa rasilimali za taifa.

“Nimejipima na nimeona ninatosha, nimekuwa kiongozi kwenye nafasi mbalimbali hata kabla ya kuingia kwenye siasa, pia ni kiongozi wa cha chama bora chenye ilani bora,” alisema mwanasiasa huyo siku ya Januari 16, jijini Dar es Salaam.

Semu anakuwa mwanasiasa wa kwanza kutoka upande wa upinzani kutangaza azma ya kuwania nafasi ya juu kabisa ya uongozi nchini Tanzania, na vivyo hivyo kukifanya ACT-Wazalendo kuwa chama cha kwanza kati ya vyama 19 vya siasa nchini Tanzania kuwaruhusu wananchama wake kutia nia na kutangaza kugombea uongozi katika Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba mwaka 2025.

TRT Afrika