Kampuni ya mawakili ya Marekani imeajiriwa na Gambia kuangalia uwezekano wa kuchukuliwa hatua za kisheria baada ya takriban watoto 70 kufariki mwaka jana kutokana na majeraha ya figo baada ya kunywa dawa za kikohozi, shirika la habari la Reuters linaripoti.
Uchunguzi ulioungwa mkono na serikali uligundua kuwa dawa zilizo ingizwa kutoka India "zina uwezekano mkubwa" kusababisha vifo vya watoto 70, wengi wao wakiwa na umri wa chini ya miaka 5 kati ya Juni na Oktoba 2022.
Madaktari wa eneo hilo walishuku dawa za kikohozi zilizo agizwa kutoka India ndizo zilizohusika. Tuhuma zao zilithibitishwa tena baada ya vipimo vya Shirika la Afya Duniani (WHO) kuthibitisha kuwepo kwa sumu hatari, na hivyo kuibua msako wa kimataifa wa kutafuta dawa hizo zilizo na madhara.
Waziri wa Sheria wa Gambia, Dawda Jallow, aliliambia shirika la habari la Reuters kuwa hatua za kisheria ni chaguo moja linalozingatiwa na serikali, ishara ya kwanza ya uwezekano wa kesi za kimataifa kuhusu vifo hivyo.
Jallow hata hivyo hajaonyesha ni nani atakayelengwa katika kesi hiyo.
Serikali ya India imesema vipimo vyake kwenye dawa hizo havikupata sumu yoyote lakini tangu wakati huo imefanya upimaji wa dawa kuwa wa lazima kwa dawa za kikohozi kabla ya kusafirishwa nje ya nchi.