Daktari huyo bingwa wa zamani, wa afya ya uzazi ya wanawake Rwanda, anatarajiwa kufikishwa mahakamani Ufaransa Jumanne.
Sosthene Munyemana anakabiliwa na mashtaka ya mauaji ya kimbari na uhalifu dhidi ya ubinadamu wakati wa mauaji ya 1994 nchini Rwanda, kwa uchunguzi uliokuwa ukiendelea kwa takriban miongo mitatu.
Munyemana alikuwa karibu na Jean Kambanda, mkuu wa serikali ya mpito iliyoanzishwa baada ya ndege iliyombeba rais wa wakati huo Juvenal Habyarimana kudunguliwa kwa kombora mnamo 1994.
Munyemana atafikishwa Mahakama ya Paris takriban miaka 30 baada ya mashtaka dhidi yake kuwasilishwa katika mji wa kusini magharibi mwa Ufaransa wa Bordeaux mnamo 1995.
Daktari huyo wa zamani mwenye umri wa miaka 68, ameishi uhamishoni Ufaransa tangu 1994.
Anashutumiwa kwa kusaini barua ya kuunga mkono serikali ya mpito, ambayo ilihimiza mauaji ya Watutsi.
Pia anatuhumiwa kwa kuwazuilia raia wa Kitutsi katika hali zisizo za kibinadamu ndani ya ofisi za serikali za mitaa ambazo alikuwa na ufunguo, mashtaka ambayo amekuwa akikanusha.
Ni kesi ya sita aina hiyo kusikizwa nchini Ufaransa dhid ya mtu anayedaiwa kuhusika katika mauaji hayo, ambapo watu wapatao 800,000, wengi wao wakiwa Watutsi, waliuawa ndani ya zaidi ya siku 100.
Mnamo 2008, Ufaransa ilikataa ombi la hifadhi la Munyemana, ambaye alifanya kazi katika hospitali ya Villeneuve-Sur-Lot kusini Magharibi mwa Ufaransa kwa muongo mmoja.
Lakini pia mwaka 2010 Ufaransa ilipinga ombi la kuhamishiwa kesi yake Rwanda baada ya mawakili wa Munyemana kudai hakuweza kupokea haki nchini humo.
Ikiwa atakutwa na hatia, huenda akahukumiwa kifungo cha maisha.
Rwanda chini ya Rais Paul Kagame imeishutumu Ufaransa kwa kutokuwa tayari kuwakabidhi kwake watuhumiwa wa mauaji ya kimbari au kuwafikisha mahakamani.
Zaidi ya watu 800,000, hasa Watutsi, waliuawa katika mauaji ya Kimbari ya Rwanda kuanzia Aprili hadi Julai 1994, kulingana na takwimu za Umoja wa Mataifa.