Kupitia mabaki hayo amefanikiwa kutengeneza makaa na mbolea bila ya kusababisha madhara kwa mazingira.
Mwenyewe aneleza kuwa ni fursa kubwa ya nishati safi inayoweza kuinua hali ya maisha ya watu nchini Congo. Wakati Destin Babila alidokeza wazo hilo kwa familia yake, wengi walimcheka wakishangaa ni kipi kizuri ambacho kinaweza kutokana na takataka.
“Takataka ni taka tu,” wengi wao walimtania lakini Destin akajitahidi kuwasisitizia kuwa kuna dhahabu kwenye taka na mabaki iwapo watu watadhubutu kuangalia na jicho la tatu.
Miaka mitatu baadae sasa ndoto yake imeanza kutimia na wakosoaji wake wameshangaa. Destin alianzisha kampuni ijulikanayo kama Wumela Biocarbon; lengo kuu likiwa ni kutumia mabaki ya mimea na taka za misitu kutengeneza makaa na mbolea. Tayari matokeo yake yameanza kuonekana kutoka kwa kampuni hio yenye wafanyakazi 12.
Mkaa utokanao na kuni ya kaboni ‘Bio-charcoal’
Destin anasema kuwa alishangaa kuona taka na mabaki mengi jijini Pointe-Noire na hakuna yeyote aliyekuwa akishughulika na hivyo basi hali hiyo ilipelekea kung’amua fursa ya kutengeneza mkaa utokanao na kaboni yaani bio-charcoal.
Je, itatengenezwa vipi?
Kuni zinapochomwa hutoa misombo yote tete iliyomo ikiwemo maji; sumu nayo hupunguzwa na kinachobaki sasa ni kaboni safi na majivu. Aidha mkaa huu huvunjika kwa urahisi na hata jivu lake halina madhara kwa mazingira kwa mkaa wenyewe ni mwepesi na rahisi kuvunjika. Matumizi ya mkaa huu ni njia moja ya kupunguza ukataji miti kiholela na hivyo basi kulinda misitu.
Usalama wa misitu na utunzaji wake
Utafiti uliofanywa na Benki ya dunia kwa niaba ya Tume ya Misitu ya Afrika ya Kati(COMIFAC) ulibaini kuwa uchomaji wa makaa ndiyo tishio kubwa la misitu katika ukanda wa Afika ya Kati. Kwa mujibu wa makadirio, zaidi ya asilimia 90 ya kuni zilizovunwa bonde la Congo zinaweza kutumika kuzalisha nishati; na mita moja ya ujazo itahitajika kwa kila mtu mmoja kila mwaka.
“Unaona sasa kwa kuzingatia takwimu hizo, basi nchi yangu hii Congo mwaka 2016 tulikaribia tani 100,000 kwenye matumizi ya makaa na nyengine tani 132,000 katika matumizi ya kuni. Kwa hivyo basi tukiamua kwa kweli tunaweza kupigana na tabia ya ukataji wa miti kiholela na mabadiliko ya tabianchi kwa ujumla.” Anasema Destine Babila.
Aidha kampuni anayomiliki Destin inazalisha mbolea ya ‘biochar’ ambayo pia inatokana na mabaki ya mimea.
“Mabaki yanachomwa katika tanuri maalum kufikia nyuzi 300 pasi na kuwepo kwa hewa. Aidha zaidi ya asilimia 85 ya kaboni vilevile inahitajika.” Anaeleza Destin.
Mbolea hii ni muhimu kwa kilimo kwani inaongeza rutuba ya udongo na kuwezesha uhifadhi wa maji kwa hadi asilimia 15 kwenye udongo. Kadhalika mbolea hii inahifadhi gesi ya carbon kwa asilimia kubwa na kuchangia kupigana na ongezeko la joto.
Ikitumika vizuri, kama anavyoeleza Destin, basi mazao yanaweza kuongezeka kuanzia asilimia 50 hadi 100.
Madai ya Destin yanathibitishwa na wataalam kutoka kwa shirika lisilo la kiserikali Pro Natura la nchini Brazil, kufuatia Kongamano la Rio mwaka 1992 ambapo malengo yalikuwa ni “Uhifadhi wa kilimo vijijini katika mataifa yanayoendelea.”
Kuongezwa kwa mbolea ya biochar kwenye udongo (kati ya gramu 300 mpaka kilo moja) kwa kila mita ya mraba kunaweza kukaboresha uzalishaji kwa asilimia 50 mpaka asilimia 200 kwa mujibu wa taarifa zilizochapishwa katika tovuti ya Pro Natura.
Aidha kutambulishwa kwa biochar katika udongo kunadumisha rutuba kwa kipindi kirefu na manufaa
- Kuchochea baiolojia ya udongo (+asilimia 40 ya mycorrhiza fungi)
- Ongezeko la kuhifadhi virutubisho (hadi asilimia 50)
- Ongezeko la uwezo wa udongo kuhifadhi maji. (hadi asilimia 18 )
- Kupunguza N2O na CH4.
Kampuni ya Wumela bio-carbon inayomilikiwa na Destin Babila inasadiki kuwa fursa ingali bado ni kubwa kutumia mabaki ya mimea na taka za misitu kuhifadhi mazingira nchini Congo.
“Nafasi na fursa bado ni kubwa mno licha ya changamoto tunazopitia zikiwemo uhaba wa fedha za kutosha kutimiza malengo yetu kama kampuni.” Anasema Destin Babila.
“Ukiangalia ulaya uwezo wa kifedha ni mkubwa lakini taka na mabaki ni finyu,; tofauti na hapa kwetu Congo mabaki na taka ni nyingi ila fedha nazo ni adimu.”