Mamia ya waasi wa Chad waliokuwa wamefungwa kwa kuhusika na kifo cha aliyekuwa rais wa nchi hiyo Idriss Deby Itno wameachiliwa baada ya miaka miwili jela.
Wanachama 380 wa kundi la waasi la Front for Change and Concord in Chad (FACT) walisamehewa na Rais wa mpito Mahamat Idriss Deby Itno mwezi uliopita.
Waziri wa Sheria wa Chad Mahamat Ahmat Alhabo, siku ya Jumatano, aliongoza hafla, ambapo alikabidhi hati za kuachiliwa kwa kundi hilo katika gereza la Klessoum karibu na mji mkuu wa N'Djamena, kulingana na Shirika la Habari la Chad.
Kuna watu 400 waliohukumiwa kifungo cha maisha Machi 21 wakihusishwa na kifo cha Idriss Deby Itno, baba wa kiongozi wa sasa wa Chad.
Walishtakiwa na kupatikana na hatia ya vitendo vya ugaidi, kudhoofisha usalama wa taifa, kuhatarisha maisha ya mkuu wa nchi na kuajiri watoto wadogo miongoni mwa mashtaka mengine.
Hatua hiyo ilikuwa ni kuwafanya watu hao ''kutafakari juu ya kitendo cha uhalifu'' ambacho walitiwa hatiani kwa mtazamo wa ''kubadilisha tabia ili kuishi maisha ya heshima ya kuwajibika baada ya kuunganishwa tena," Alhabo alinukuliwa akisema.
Kuachiliwa kwa kundi hilo ni katika "kutimiza ahadi ambayo rais aliitoa mwaka jana katika mazungumzo ya kitaifa ya kujenga amani kwa kuwaachilia huru wanachama wa makundi yenye silaha chini ya msamaha ili kuendeleza mazungumzo."
Kiongozi wa kundi hilo Mahamat Ali Mahadi, ambaye alihukumiwa kifungo cha maisha bila kuwepo, alitengwa na msamaha huo.
Chad ilitoa hati ya kimataifa ya kukamatwa kwa Mahadi.
Mnamo Januari 2022, serikali ya mpito pia iliwaachilia wanachama 250 wa vikundi vyenye silaha ambao walikuwa wamepatikana na hatia kwa tuhuma za kuchukua silaha dhidi ya serikali.
Waasi wa FACT walioachiliwa Jumatano walikamatwa Aprili 2021 wakati wa mapigano na wanajeshi kaskazini mwa Chad.
Baba yake Deby, ambaye alitawala nchi hiyo kwa miongo mitatu, aliuawa katika mapigano hayo alipoenda kuwatembelea wanajeshi waliokuepo mstari wa mbele.
Baraza la kijeshi lililoongozwa na mwanae Mahamat Deby liliundwa kutawala nchi kwa kipindi cha mpito cha miezi 18.
Alitakiwa kukabidhi madaraka kwa serikali iliyochaguliwa Oktoba mwaka jana, lakini muda huo haukutimizwa na akawa rais wa mpito mwezi huo huo.
Jeshi limeongeza muda wa mpito kwa miaka miwili, huku uchaguzi ukipangwa kufanyika Oktoba 2024, suala ambalo limesababisha maandamano ya vurugu mitaani.