Samia Suluhu Hassan akitoa heshima zake za mwisho kwa Marehemu Edward Lowassa mjini Atrusha Tanzania / Picha : Ikulu Tanzania 

Mungu amefanya kazi yake, tumhidi mwenyezi Mungu. Maneno yenye machungu na huzuni yakitamatisha hotuba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan alipohudhuria mazishi ya hayati Waziri Mkuu mstaafu EDward Lowassa.

Rais Samia alisema Tanzania imepoteza mwanasiasa aliyepigania mageuzi ya taifa.

''Kama taifa tumepoteza moja ya viongozi mahiri, mpenda maendeleo, mwana mageuzi na kipenzi cha wengi,'' alisema Rais Samia katika hotuba yake. ''Natoa pole kwa wana Monduli na kwa wanachi wote wa Tanzania kwa msiba huu mzito,'' aliendelea kusema.

Samia Suluhu hassan anasema amejifunza ushupavu, ulezi na ustahamilivu kutoka kwa Lowassa / Picha: Ikulu Tanzania 

Rais Samia alimsifia Hayati Lowassa kwa kujitolea nusu ya maisha yake katika utumishi wa umma na kuitumikia serikali ya Jamhuri ya Tanzania.

''Amejitolea muda na maisha yake kwa ajili ya nchi yake na kubeba dhamana ya uongozi katika kila alichokabidhiwa,'' Rais Samia alisema.

Rais Samia ataja vitatu alivyojifunza kwa Lowassa

  • Ushupavu

Rais Samia amemtaja Edward Lowassa kama kiongozi jasiri na shupavu , sifa alizoonyesha wakati mbali mbali katika uongozi wake. Alisimamia masuala yaliyokubalika ndani ya serikali na yaliyoagizwa na chama bila kununa.

Rais Samia alitaja muda wake Marehemu Lowassa kama waziri wa maji, alipozuiwa kuyatumia maji ya ziwa Victoria kwasababu za kihistoria lakini alitumia ujasiri na ushupavu wake kuishauri serikali na kuweka misukumo iliyowezesha maji ya ziwa Victoria kutumika katika mikoa ya Shinyanga na Tabora.

  • Ulezi

Rais Samia alisema hakuna mwisho wa idadi ya waliofaidi kutokana na malezi ya marehemu Edward Lowassa, akitaja nyumbani kwake, mkoani, serikalini hadi chamani CCM na hata upande wa upinzani alipojiunga nao. Rais alisema Lowassa aliwalea na kuwaongoza vijana wengi ambao wanaendelea kuitumikia taifa.

''Sifa hii ya ulezi ilimjengea umaarufu na mapenzi makubwa miongoni mwa wengi,'' alisema Rais Samia.

Rais Samia alisema Ulezi wa Lowassa ulidhihirika wazi alipokuwa akigombea urais, ambapo ajenda yake kubwa aliyosukuma ilikuwa elimu, elimu na elimu.

  • Ustahamilivu

Rais Suluhu pia alisema amejifunza ustahamilivu kutoka kwa Lowassa. Katika mapito yake kisiasa, Lowassa alihama kutoka Chama Cha Mapinduzi ambacho alikuwa mwanachama kwa muda mrefu, na kukihamia chama cha upinzani CHADEMA.

Rais Samia alimsifu Lowassa kwamba alipoteuliwa kuwa mgombea wa urais kwa tikiti ya chama hicho, aliendelea kunadi sera zake na kufafanua dhana yake ya safari yake ya matumaini bila kumtukana, kumkejeli au kumzushia mtu yeyote.

''Hata aliporudi CCM, hakuwahi kuwananga, kuwazodoa na kuwakebehi au kuwasema vibaya kule alikotoka upinzani,'' aliendelea kusema Rais Samia.

Edward Ngoyai Lowassa amezikwa nyumbani kwake Monduli Mkoani Arusha katika shughuli iliyohudhuriwa na viongozi mbali mbali wa dini, serikali na upinzani. / Picha : Ikulu Tanzania 

Kwa upande wake kiongozi wa upinzani nchini Tanzania Freeman Mbowe ambaye pia alihudhuria mazishi ya marehemu Lowassa alimsifia kama kiongozi aliyejenga demokrasia ya nchi kwa viwango ambavyo havijafikiwa na mwanasiasa mwengine.

''Lowassa alikuwa mtu wa karama ya ajabu, aliyeweza kuunganisha makundi mbalimbali wakati wote,'' alisema Mbowe. ''Huyu ni mtu aliyeleta kasi ya ukuaji wa demokrasia katika nchi yetu,'' aliongeza Mbowe.

Hayati Lowassa alizikwa yumbani kwake Monduli Mkoani Arusha Jumamosi tarehe 17 Februari, 2024.

Edward Lowassa alifariki Dunia February 10,2024 katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete Jijini Dar es Salaam baada y akuugua kwa muda.

Lowassa aliyefariki akiwa na miaka 70, alikuwa Waziri Mkuu wa Tanzania kuanzia mwaka 2005 hadi 2008, akiwa chini ya Rais Jakaya Kikwete.

TRT Afrika