Kiongozi wa Baraza Kuu la Sudan amesema kurejea katika hali ya kabla ya vita na wapinzani wa Rapid Support Forces (RSF) haiwezekani.
Abdel Fattah al-Burhan alitoa kauli hiyo siku ya Jumanne katika hotuba yake kwa njia ya televisheni iliyopeperushwa na televisheni ya taifa ya Sudan katika maadhimisho ya miaka 69 ya uhuru wa nchi hiyo kutoka kwa uvamizi wa Uingereza.
Hata hivyo, alionyesha utayari "kushiriki katika mpango wowote wa kweli ambao unamaliza vita na kuhakikisha kurudi salama" kwa raia kwenye makazi yao.
"Hali haiwezi kurejea jinsi ilivyokuwa kabla ya Aprili 15, 2023, wala hatuwezi kukubali kuwepo kwa wauaji hawa, wahalifu, na wafuasi wao miongoni mwa watu wa Sudan tena," Burhan alisema akimaanisha kundi la RSF.
Aliongeza kuwa watu wa Sudan wanakabiliwa na mauaji, njaa, kufukuzwa na ukiukwaji wa sheria na wanamgambo wa RSF.
Vita vya wenyewe kwa wenyewe Sudan
Takriban watu 25,000 wameuawa na zaidi ya milioni 10 wamekimbia makazi yao tangu Aprili 2023, wakati vita vya kupagania madaraka vilipozuka kati ya jeshi la Sudan linaloongozwa na Jenerali Abdel Fattah al-Burhan na RSF inayoongozwa na makamu wake wa zamani Mohamed Hamdan Dagalo.
Mapigano hayo yameenea katika majimbo 13 kati ya 18 ya Sudan, na kusababisha uharibifu mkubwa na kusukuma mamilioni kwenye ukingo wa njaa na vifo.
Juhudi za upatanishi zinazoongozwa na nchi kadhaa, ikiwa ni pamoja na Marekani na Saudi Arabia, bado hazijafanikiwa kupata usitishaji mapigano huku kukiwa na shutuma za kufelisha juhudi hizo kutoka kwa jeshi la Sudan na RSF.