Watu 22 walifariki baada ya boti mbili zilizokuwa zimebeba wahamiaji kupinduka katika pwani ya Madagascar katika Bahari ya Hindi, afisa mmoja alisema Jumamosi.
Balozi wa Somalia nchini Ethiopia na Umoja wa Afrika Abdullahi Warfa aliiambia Radio Mogadishu inayoendeshwa na serikali kwamba boti hizo zilikuwa na abiria 70 - wote wakiwa raia wa Somalia.
Hakutaja tarehe ya tukio lakini alithibitisha kuwa miili ilipatikana Jumamosi.
Alisema abiria 48 waliokolewa na wavuvi na kupelekwa kwa matibabu.
Kuongezeka kwa vifo vya wahamiaji
“Uchunguzi unaendelea na tunayo majina ya waathiriwa na tutawaeleza kupitia wizara ya mambo ya nje,” alisema.
Serikali haikueleza kwa kina chanzo cha ajali hiyo.
Bahari ya Hindi imeshuhudia ongezeko la vifo vya wahamiaji mnamo 2024.
Takriban watu 24 walikufa baada ya mashua kuzama katika ufuo wa Visiwa vya Comoro, Shirika la Kimataifa la Uhamiaji (IOM) lilisema mapema mwezi huu.
Shirika hilo la Umoja wa Mataifa limesema wanawake, watoto na watoto wachanga ni miongoni mwa waathiriwa na kwamba boti hiyo ilipinduliwa kimakusudi na wasafirishaji haramu.
Mnamo Septemba, mashua iliyokuwa na watu 12, ikiwa ni pamoja na watoto wawili na mama mjamzito, iliondoka pwani ya Anjouan katika mlolongo wa kisiwa cha Comoro na haikufika Mayotte, kisiwa cha visiwa vya Comoro na idara ya Ufaransa tangu 2011.
Na watu wanane waliuawa mwezi Agosti katika tukio sawa, ikiwa ni pamoja na mvulana wa miaka 12.
Maelfu ya wahasiriwa wamekufa kwenye njia ya uhamiaji ya Bahari ya Hindi katika jaribio la kufikia kisiwa kinachozozaniwa cha Mayotte.