Mary alijifungua mtoto wa kwanza mwaka 2021. Kujifungua kwake kulimleta uso kwa uso na huzuni kubwa iliyokuja punde baada ya kuzaa.
Kabla ya kujifungua mwanamke huyo wa kitanzania alikuwa mchangamfu, anayejali na mwenye urafiki wa hali ya juu.
Kisha siku moja - baada ya kujifungua - Mary alijitenga, akiongea peke yake mara nyingi tu.
“Nilikuwa nikiongea peke yangu kimyakimya, nilijiona kuwa sifai, na sikuweza kuzungumza na mtu yeyote jinsi nilivyohisi.
Tabia yake ambayo ilitazamwa kuwa ya ajabu na ndugu zake ilipelekea kukosolewa sana.
"Shangazi alisema mimi ni mkorofi alinishutumu kwa kuwadharau mpaka alinikejeli ninajeuri kana kwamba mimi ndiye mtu wa kwanza kupata mtoto" anaongeza Mary
Hata hivyo anaongeza kuwa hakuna aliyekuwa anamuelewa.
"Nilijiona mpweke moyoni mwangu, nilihisi kuvunjika, kupotea na kuwa peke yangu. Nilitumia saa nyingi kwenye simu yangu na kulala ilikuwa ngumu,”
Msichana huyo mwenye umri wa miaka 29 baadaye alipata usaidizi kutoka kwa rafiki yake ambaye pia alikuwa amepatwa na mfadhaiko baada ya kuzaa - aina ya msongo anaopata mama baada ya kujifungua kutokana na mabadiliko ya homoni na kisaikolojia.
“Rafiki yangu aliniomba nitafute msaada wa kimatibabu. Hata alinielekeza kwa daktari aliyemsaidia kushinda hali yake,” Mary anasema.
Isaac Lema, mwanasaikolojia katika Idara ya Afya na Magonjwa ya Akili katika Hospitali ya Taifa Muhimbili nchini Tanzania, anasema wakati mwingine watu hupitia kipindi cha ugonjwa wa akili ambacho “bila wao kuelewa”.
Hali ilivyo duniani kuhusu afya ya akili
Wanaharakati, mashirika ya kimataifa, viongozi wa dini na hata wasanii kote duniani wamekua wakishiriki katika kuelimisha na kuufahamisha umma kuhusu changamoto hii ambayo ni kama imepigiwa msumari katika kipindi ambacho dunia inapambana na maradhi ya Corona.
Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani-WHO, watu takribani bilioni moja wana tatizo la afya ya akili. Inafafanuliwa zaidi kuwa katika kila vijana 7 mmoja tayari ana aina fulani ya tatizo la afya ya akili.
Baadhi hufananisha matatizo haya ya afya ya akili na imani za kishirikina, wengine wanasema ni makusudi tu, huku baadhi wakitumia maneno mazito kama vile 'utahira' au 'uchizi'. Hali inayopelekea wengi kuhofia kutafuta msaada kwa kuogopa kuonekana wamechanganyikiwa.
''Kutengwa kwa jamii, hofu ya magonjwa na kifo, na hali mbaya ya kiuchumi na kijamii inayohusishwa na janga la COVID-19 imechangia kuongezeka kwa 25% ya unyogovu na wasiwasi ulimwenguni,'' WHO ilisema mwaka jana.
Kulingana na shirika la afya ulimwenguni pote, “mmoja kati ya kila vijana saba tayari ana aina fulani ya tatizo la kiakili.”
Mnamo mwaka wa 2019, kujiua kulichangia zaidi ya kifo kimoja kati ya 100 na asilimia 58 ya watu waliojiua walitokea kabla ya umri wa miaka 50 na shida za afya ya akili kuwa moja ya vichochezi, WHO ilisema katika ripoti.
Afya ya akili ni kwa kila mmoja uwe umegundulika na ugonjwa wa akili au haujagundulika kuwa na ugonjwa bado unahitaji afya ya akili, anasema Daktari Isack Lema
Anasisitiza kuwa afya ya akili sio kukosa akili kama ambavyo watu hudhani. Anasema mtu hawezi kukosa akili kikubwa ni je hiyo akili aliyonayo ipo katika afya duni au afya bora.
“Kuwa na akili yenye afya bora ni pale mtu anapokuwa na uwezo wa kutumia akili yake kudhibiti msongo, hisia, kufanya kazi kujifunza na kuongeza mchango katika jamii,” anaongeza mtaalamu huyo.
Unajuaje kama wewe, ndugu au jirani yako ana tatizo la afya ya akili?
Mtaalamu huyo wa saikolojia anasema vipo viashiria ambavyo vinaweza kukusaidia kujitambua wewe au jirani kama na kiwango cha juu cha msongo au tatizo la afya ya akili.
"Moja ni mtu au wewe mwenyewe kuonyesha hali yoyote ya kukata tamaa. Mtu ambaye anapenda kujichanganya au kujumuika lakini ghafla hajumuiki na watu tena" anasema Lema
Vilevile ameshauri kuwa makini na watu unapozungumza nao kwani kuna wale ambao unaweza kusikiliza mazungumzo yao ukagundua wana mawazo ya kutaka kujidhuru au kumdhuru mtu mwingine.
Na endapo katika upande wa hisia, mtu anashindwa kudhibiti hasira zake. Kwa mfano, jambo dogo analikuza au anaonyesha mwitikio mpaka wengine wanashangaa.
Lakini pia waweza kugundua endapo ukienda kulala hupati usingizi vizuri.
Pia mtu ambaye amekaa kwenye huzuni kwa muda mrefu kupita muda wa kawaida ambao mtu yoyote anaweza akapona na kuendelea na shughuli zake.
Mwisho ni hali ya uoga au wasiwasi usio wa kawaida ni miongoni mwa ishara za mtu mwenye tatizo la afya ya akili.
Historia ya matatizo ya afya ya akili?
Watu wengi wanachanganya afya ya akili na magonjwa ya akili. Lema anasisitiza kuwa, “Afya ya akili sio udhaifu kwa hiyo mtu anapoonekana dhaifu hainaanishi ana tatizo la afya ya akili”.
"Magonjwa ya akili yanatokana na mwingiliano wa vinasaba yaani jenetiki na mazingira aliyonayo mtu. Na mwingiliano huo humuweka mtu katika hali hatarishi ya kupata magonjwa ya akili" anasema mtaalamu
"Hii huathiri tabia, mtu anavyo fikiri, anavyo hisi lakini pia mwitikio wa mwili. Kwani mtu aliyezaliwa kwenye familia iliyo na historia ya ugonjwa wa akili atakua na hali hatarishi kuliko yule ambaye hajazaliwa katika familia hiyo"
Pia kuna mazingira ambayo yanakua ni kichocheo cha kupata mlipuko wa ugonjwa wa akili. Anasema ugumu wa maisha, kupanda kwa bei ya chakula, yote haya yanapandisha kiwango cha msongo.
Kiwango cha juu cha msongo wa mawazo pia hupelekea matatizo ya afya ya akili. Na mtu mwenye hali hii huwa amekata tamaa kabisa, amekosa dira na anaweza kusema kabisa kuwa amevurugwa. Inapofikia hivyo, hicho kinakuwa ni kiwango cha juu na hatimae kupelekea matatizo ya afya ya akili.
Je nini cha kufanya ili kujikinga na matatizo ya afya ya akili?
Mwanasaikolojia tiba kutoka Idara ya Afya na Magonjwa ya Akili kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili anasema kuna umuhimu wa kuwa na huduma kinga katika kukabiliana na matatizo haya kwani ni vitu ambavyo watu wanaweza kuvifanya na gharama yake si kubwa ukilinganisha na gharama ya matibabu inayotoka hospitali.
Hapa anamaanisha mambo kadhaa yanayoweza kumsaidia mtu kuepukana na tatizo la afya ya akili.
Mazoezi: Anasema ni vyema kushughulisha mwili kwani wakati huo wa mazoezi humsaidia mtu kuondoa msongo. Hapa anazungumzia mazoezi mbalimballi ikiwemo yale ya kuvuta pumzi na kutoa, kulegeza mwili na kadhalika.
Kupumzika: Anasema wengi hupumzika baada ya kuchoka lakini hii si sahihi. Unatakiwa kupumzika kama sehemu ya ratiba yako uwe umechoka au hujachoka. Kama vile mapumziko yanavyowekwa shuleni. Watu ni lazima wajiwekee ratiba ya kupumzika hata maeneo ya kazi na si kusubiri uchovu.
Chakula: Hapa mtu anapaswa kula chakula sahihi, yaani mlo kamili lakini pia kuzingatia muda au wakati wa kula ulio sahihi bila kusahau kipimo yaani kula kwa kiasi.
Msaada wa kijamii: Pata muda wa kukaa na wapendwa wako, yaani jumuika na jamii inayokuzunguka na hapa si kupitia mtandao pekee bali kuonana na watu ana kwa ana. Kwani kukaa pamoja itamfanya mtu ajione sehemu ya jamii na ushiriki wake unathaminiwa. Epuka kujitenga.
Shirikisha wengine inapobidi: Zungumza na watu hasa unapoona kiwango chako cha msongo kinakuja juu. Pia unaweza kuomba msaada ili mambo yaende.
Tatua matatizo jinsi yanavyo kuja: Hapa anasisitiza usiache matatizo yarundikane. Acha kabisa kusikilizia matatizo. Utafanya yawe makubwa na utashindwa kutatua. Hivyo ni muhimu kujifunza mbinu za utatuzi wa matatizo kwa wakati.
Mwisho jipe muda wa kupona na kurejea kabla hujaanza kukabiliana na mambo mengine.
Madhara yatokanayo na afya ya akili ni makubwa, kuanzia kiafya, kielimu na hata kiuchumi huku athari kubwa zaidi ikiwa ni kupoteza uhai wa watu kutokana na matukio yanayo sababishwa na maradhi ya afya duni ya akili.
Hata hivyo, wataalamu wanasema kinga ni bora kuliko tiba huku rai ikitolewa kwa yeyote anaye hisi kuelemewa kutafuta msaada kwa watu wakaribu na hasa wataalamu wa afya.