Ripoti iliyotolewa na Shirika La afya duniani WHO, inaashiria kuwa nchi kadhaa Afrika Mashariki zitaathiriwa zaidi upande wa afya kutokana na Elnino.
El Nino ni hali ya kuongezeka kwa mvua kupita kiasi cha kawaida.
"Nchi zilizo katika hatari kubwa ya mafuriko zitakabiliwa na hatari ya kuongezeka kwa magonjwa ikiwemo Kipindupindu na Malaria," WHO imesema katika ripoti yake mpya.
"Katika sehemu kubwa ya Afrika Mashariki, El Nino inahusishwa na mvua kubwa kuliko ya kawaida, na hatari ya mafuriko, kuanzia karibia mwezi Oktoba," ripoti hiyo inasema.
"Utabiri wa sasa wa msimu - wakati bado hauna uhakika katika hatua hii - unaonyesha kuwa mabadiliko haya yanaweza kutokea zaidi kusini mwa Ethiopia, sehemu za Tanzania, Kenya na Somalia, na pia kwa kiwango kidogo nchini Burundi, Rwanda na Uganda, " ripoti imeongeza.
Wataalam wanasema Sudan Kusini yenyewe haitapatwa na mvua nyingi wakati wa El Nino, lakini mvua kubwa ya Machi/ Aprili imeathiri ziwa Victoria ambayo ni chanzo kikuu cha maji ya Mto White Nile, unaovuka Sudan Kusini.
Ripoti inaonya kuwa ikiwa mvua ya Oktoba-Desemba ni juu ya wastani juu ya bonde la Ziwa Victoria, basi kiwango hicho cha ziwa kitaongezeka zaidi, na kusababisha kufurika kwa mto chini ya mteremko wake, na kusababisha watu kuhama makazi yao, pamoja na kupoteza mazao na mifugo.
Nyingi za nchi hizo zinazokabiliwa na hatari ya mvua kubwa baadaye mwakani tayari zinaripotiwa zimekabiliwa na viwango vya juu vya mafuriko mwaka huu.
Hasa, katika sehemu za Sudan Kusini, hii inasemekana inaweza kusababisha mwaka wa tano mfululizo mafuriko yaliyoenea sana, na kusababisha hasara ya mazao na mifugo.
Rwanda ilkumbwa na mafuriko Mei mwaka huu ambayo ikiuwa watu 100.
Hatari ya kiafya kwa nchi zitakazopata el nino
Shirika la afya duniani linaonya kuwa nchi zitakazoathiriwa na mvua za El nino zitapata shida hizi za afya :
- Utapiamlo
- Kipindupindu na magonjwa mengine ya kuhara
- Homa ya matumbo
- Homa ya Ini (Hepatitis A na E)
- Malaria
- Homa ya Chikungunya - ugonjwa unaoenezwa na mbu wenye virusi hivi na dalaili zake ni pamoja homa, kichefuchefu , maumivu ya kichwa, homa kali, kupata maumivu ya viungo hasa miguu an mikoni kuwa na uchovu wa mwili
- Homa ya Dengue - ugonjwa wa kitropiki unaosababishwa na virusi vya dengue