Marais wa Rwanda Paul Kagame na DRC Felix Tshisekedi

Mawaziri wa mambo ya nje wa Afrika Kusini na Rwanda walifanya mazungumzo kwa njia ya simu Alhamisi ili kutuliza uhasama baada ya rais wa Rwanda Paul Kagame, kuwashutumu viongozi wa Afrika Kusini kutatiza mijadala kuhusu mzozo wa mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Afrika Kusini Ronald Lamola na Waziri wa Mambo ya Nje wa Rwanda Olivier Nduhungirehe walikubaliana kuendeleza mazungumzo kuhusu mgogoro wa Congo wakati wa mawasiliano yao kwa njia ya simu.

"Tulieleza nia yetu ya kuendeleza mazungumzo mashariki mwa DRC na tukakubaliana na mpango wa kusitisha mapigano," Lamola aliandika kwenye mtandao wa X, akimaanisha mipango ya amani ya kikanda.

Juhudi za kidiplomasia zinafuatia ukosoaji mkali kutoka kwa Rais wa Rwanda Paul Kagame, ambaye alimshutumu Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa kwa "mashambulizi ya makusudi" na "uongo" kuhusiana na majadiliano yao ya awali.

Kagame alihoji kuhusu jukumu la vikosi vya Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) nchini DRC, akivieleza kama "kikosi cha vurugu" badala ya kutafuta amani.

"Ikiwa Afrika Kusini itapendelea makabiliano, Rwanda itashughulikia suala hilo katika muktadha huo siku yoyote," alionya mapema.

Kundi la waasi la M23 lilianzisha mashambulizi makubwa wiki iliyopita katika mji wa kimkakati wa Goma, ambao ni makazi ya watu takriban milioni 3.

DRC hata hivyo, iliishutumu Rwanda kwa kutuma wanajeshi katika mji huo kusaidia waasi.

Wakati Rwanda ikikanusha kuwaunga mkono waasi, viongozi wa eneo hilo wametoa wito wa kusitishwa mara moja kwa mapigano huku watu kadhaa wakiuawa na mamia wengine kujeruhiwa.

TRT Afrika