Si mara ya kwanza Afrika Kusini kujaribu kujiondoa kutoka ICC / Photo: AP

Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa anasema chama chake tawala cha ANC kimeazimia kuwa nchi hiyo inapaswa kujiondoa katika Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC).

"Ndiyo, chama tawala... kimechukua uamuzi huo kwamba ni jambo la busara kwamba Afrika Kusini inapaswa kujiondoa katika ICC," Ramaphosa alisema wakati wa mkutano na waandishi wa habari ulioandaliwa pamoja na Rais wa Finland Sauli Niinisto anayezuru Jumanne.

Ramaphosa alisema uamuzi huo, ambao unafuatia mkutano wa mwishoni mwa wiki wa African National Congress (ANC), ulifikiwa "kwa kiasi kikubwa" kwa sababu ya kile kinachoonekana kama unyanyasaji wa mahakama kwa baadhi ya nchi.

“Tungependa suala hili la kutotendewa haki lijadiliwe ipasavyo, lakini kwa sasa chama tawala kimeamua kwa mara nyingine kujitoa,” alisema.

Tangazo la Afrika Kusini linakuja wakati shinikizo likianza kuongezeka kwa nchi hiyo kuchukua hatua juu ya hati ya kukamatwa kwa ICC dhidi ya Rais wa Urusi Vladimir Putin.

Afrika Kusini inatazamiwa kuwa mwenyeji wa mkutano wa kilele wa jumuiya ya kiuchumi inayojulikana kama BRICS - yenye Brazil, Urusi, India, China na Afrika Kusini - Julai mwaka huu huku Putin akitarajiwa kuhudhuria.

"Ndiyo, chama tawala... kimechukua uamuzi huo kwamba ni jambo la busara kwamba Afrika Kusini inapaswa kujiondoa katika ICC,"

Cyril Ramaphosa, Rais wa Afrika Kusini

Hati ya kukamatwa kwa Putin ilifuatia shutuma kwamba Kremlin iliwafukuza watoto wa Ukraine kinyume na sheria.

Nchi ambao ni wanachama wa ICC wanatakiwa kumkamata mtu anayetafutwa na mahakama mara tu mtu kama huyo atakapoingia katika eneo lao.

Kuhusu iwapo Afrika Kusini ingemkamata Putin, Ramaphosa alisema "suala hilo linazingatiwa".

Nchi yenye nguvu katika bara, Afrika Kusini imekataa kulaani uvamizi wa Ukraine ambao kwa kiasi kikubwa umeitenga Moscow katika jukwaa la kimataifa, ikisema inataka kutoegemea upande wowote na inapendelea mazungumzo kumaliza vita.

Si mara ya kwanza Afrika Kusini kujaribu kujiondoa kutoka ICC.

Ilifanya jaribio mwaka 2016 kufuatia mzozo mwaka mmoja kabla wakati Rais wa Sudan Omar al-Bashir alipotembelea nchi hiyo kwa ajili ya mkutano wa Umoja wa Afrika.

Ilikataa kumkamata licha ya kiongozi huyo wa wakati huo kukabiliwa na hati ya kukamatwa ya ICC kwa madai ya uhalifu wa kivita.

Uamuzi wa kutatanisha wa kujiondoa hata hivyo ulibatilishwa wakati mahakama ya ndani ilipoamua kuwa hatua hiyo ingekuwa kinyume cha katiba.

TRT Afrika na mashirika ya habari