Mkurugenzi Mkuu wa Vituo vya uthibiti wa Magonjwa Afrika , yaani Africa CDC Dkt. Jean Kaseya amesema kuwa hatari ya maambukizi ya Marburg yamepungua kabisa nchini humo,
"Nilichoona Rwanda ni karibu na hatari kukwisha kabisa. Nasema 'karibu ' kwa sababu hatuwezi kusema ni asilimia 100. Lakini naweza kusema na nina uhakika asilimia 95 kwamba hakuna hatari kwa Rwanda kueneza ugonjwa nje. " alisema wakati wa mkutano na waandishi wa habari mtandaoni Alhamisi, Oktoba 10.
Marburg (MVD) ni homa hatari ya kuvuja damu isiyo na chanjo au tiba inayojulikana na imeweka ulimwengu kwenye tahadhari ya afya na wanasayansi walikuwa wakiharakisha kutafuta chanjo.
Rwanda ilitangaza mlipuko wa Marburg mwezi Septemba.
Kufikia 10 Oktoba 2024, wizara ya afya ilitangaza kuwa watu 58 walikuwa wameambukizwa na Marburg huku 13 wamepoteza maisha yao tangu mlipuko huo.
Kaseya ambaye alisafiri kwenda Rwanda hivi karibuni alipongeza hatua za kuzuia maambukizi nchini humo ikiwa ni pamoja na jinsi taasisi mbalimbali zikiwemo polisi, vituo vya afya na maofisa wa uchukuzi wanavyofanya kazi kwa pamoja.
"Watu huko wanaweza kupata ambulensi popote nchini, si Kigali pekee. Na wanaweza kupeleka wafanyakazi wa afya kwa wakati ufaao," alisema huku akipongeza utaratibu uliopo wa kufuatilia na kufuatilia mawasiliano ili maambukizi yasiotoke nje ya Rwanda.
"Hii inashangaza kwa sababu wanafuatilia mawasiliano haya kila siku. Nataka pia kusema kwamba Rwanda inatumia uwazi katika mlipuko huu," alisema, huku akihoji kuwa nchi hiyo haipaswi "kuadhibiwa" na marufuku ya usafiri.
" Kukaribia kutokomezwa kwa virusi hivyo kunaashiria mafanikio makubwa kwa mfumo wa afya wa Rwanda, ambao umekuwa ukifanya kazi kwa karibu na washirika wa kikanda na kimataifa kudhibiti ugonjwa huo. Maendeleo haya yanatoa hakikisho kwa nchi jirani na kuangazia utayari wa Rwanda katika kushughulikia milipuko ya virusi vyovyote," aliongenza.
Hadi sasa watu 346 wamepata chanjo ya majaribio dhidi ya marburg.